Majaliwa kuzindua tuzo ya kwanza ya uhifadhi na utalii

Arusha. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kesho Ijumaa anatarajiwa kuzindua tuzo ya kwanza ya uhifadhi na utalii nchini.

Imeelezwa kuwa tukio hilo linalenga kutambua mchango wa watu na taasisi binafsi zilizoleta mafanikio katika sekta hiyo muhimu nchini.

Uzinduzi wa tuzo hizo za kimataifa utakaofanyika kesho Ijumaa Desemba 20, 2024 jijini Arusha, umeandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kwa mwaka huu, jumla ya tuzo 11 za awali zitatolewa kama ishara ya kuanzisha utaratibu wa kuadhimisha hafla hiyo kila mwaka.

Miongoni mwa watakaotunukiwa tuzo ni Rais Samia Suluhu Hassan, atakayepokea Tuzo ya Uongozi wa Heshima kwa maono yake katika mafanikio ya sekta ya utalii, hasa kupitia filamu ya The Royal Tour na Kampeni ya Amazing Tanzania.

Wanajiolojia maarufu, Dk Louis Leakey na Mary Leakey, pia watatambuliwa kwa ugunduzi wa kihistoria wa fuvu la mtu wa kale na nyayo za Laetoli katika Bonde la Ngorongoro, ugunduzi ambao umeiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia.

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Arusha leo Alhamisi Desemba 19, 2024, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi, amesema tukio hilo litahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

“Siku hii itakuwa ya kipekee kutambua watu na taasisi ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya sekta ya utalii na uhifadhi,” amesema Dk Abbas.

Kwa mujibu wa Dk Abbas, sekta ya utalii imepiga hatua kubwa kwa kuingiza zaidi ya Dola 3.534 bilioni hadi Julai 2024, na idadi ya watalii kufikia milioni mbili.

“Tanzania inalenga kufikia watalii milioni tano na mapato ya Dola 6 bilioni ifikapo 2025,” amesema Dk Abbas.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Wilbard Chambulo akizungumzia tuzo hizo, amepongeza hatua hiyo ya Serikali na kusisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu ya barabara na mageti ndani ya hifadhi ili kuimarisha huduma kwa watalii.

Tuzo hizi zinatarajiwa kuleta hamasa mpya kwa wadau wa sekta ya utalii kuongeza juhudi katika kufanikisha malengo ya Serikali na kukuza taswira ya Tanzania kimataifa.

Related Posts