Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA).
Maadhimisho hayo yatafanyika kwa siku tano kuanzia Januari 19 hadi 23, 2025 jijini Arusha.
Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Barke Sehel amesema wamemuomba Rais kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo.
Amesema siku hiyo masuala mbalimbali yatajadiliwa, yakiwamo ya haki na usawa wa kijinsia.
Jaji Sehel amezungumzia kesi za ubakaji na ulawiti, akisema kwa miaka ya hivi karibuni zimeongezeka.
“Kwenye maadhimisho haya tutaeleza changamoto mbalimbali, ikiwamo hii ya ongezeko la kesi za ubakaji na ulawiti na nini kifanyike,” amesema.
“Miaka ya nyuma kesi za namna hii zilisikika kwenye baadhi ya mikoa, lakini miaka ya karibu mikoa yote ina matukio haya tena kwa kiwango cha juu,” amesema.
Ameeleza: “TAWJA tunafanya jitihada kuhakikisha changamoto hizi zinatatuliwa katika nyanja mbalimbali ikiwamo kutoa elimu kwenye masuala ya usawa wa kijinsia.”
Akizungumzia miaka 25 ya chama hicho, Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo taifa, Sophia Wambura amesema katika kipindi hicho TAWJA imefanikiwa kukuza hali ya usawa kwenye ngazi ya utendaji wa Mahakama.
“Vilevile tumehamasisha usawa kwenye jamii katika kuijengea uwezo kutambua haki zao katika mirathi, talaka, haki za usawa na masuala mengine ya kijamii,” amesema.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na mwenyekiti wa kamati mwenyeji ya maandalizi ya maadhimisho hayo, Aisha Bade amesema bado kuna changamoto katika dhamana.
Amesema pamoja na kwamba dhamana zinakua wazi lakini wahusika wanashidwa kutimiza masharti kwa kukosa baadhi ya mahitaji kama vile mdhamini na vitambulisho, jambo ambalo katika maadhimisho hayo pia watatoa elimu.
Maadhimisho hayo yatashirikisha wadau wengine ikiwamo majaji na mahakimu wanawake kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Pia watakuwapo washirika wa kimataifa kama UN Woman, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef).