Shule 26 zapata Tuzo ya Bendera ya Kijani

Morogoro. Jumla ya shule 26 za msingi na sekondari katika halmashauri nne zimetunukiwa Tuzo ya Bendera ya Kijani kutoka Taasisi ya Elimu ya Mazingira Duniani (FEE) baada ya kukidhi vigezo vya kuboresha elimu na mazingira kupitia Programu ya Eco-School unaosimamiwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) hapa nchini.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa tuzo ya bendera ya kijani wilayani Mvomero, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Zainab Katimba amesema walimu, wanafunzi, jamii na wataalamu wana kila namna ya kuhakikisha miti inayopandwa katika maeneo mbalimbali nchini inatunza ili kudumisha uhifadhi wa ardhi na mazingira kwa ujumla.

Zainab amesema halmashauri nne ambazo zimepata tuzo ya bendera ya kijani zihakikishe shule zao hazisirudi nyuma katika jitihada za kutunza na kuhifadhi mazingira ili kuendelea kuwa somo kwa shule nyingine na taifa kwa ujumla.

“Mkoa wa Morogoro ambao una idadi kubwa ya shule zilizonufaika ziweke utaratibu wa kusambaza maarifa ya programu hii kwa shule zote za msingi na sekondari na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Tamisemi kila baada ya miezi sita lakini tuzichukulie changamoto kama fursa ya kufanya vizuri zaidi na endeleeni kushirikiana na jamii na kufanya kazi kama timu ili kuyatunza mazingira yetu,” amesema Zainab.

Mkurugenzi Mtendaji shirika la kuhifadhi misitu ya asili Tanzania (TFCG), Charles Meshack amesema kupitia Programu ya Eco-Schools imewezesha shule 22 za msingi na nne za sekondari imewezesha Tanzania kupata tuzo ya bendera za kijani katika halmashauri ya Mvomero, Morogoro, Kilosa na Mufindi ikitajwa tuzo hiyo ikielezwa kuipa heshima nchi.

“Programu ya Eco-schools inatekelezwa katika nchi 87 duniani na hii programu inazingatia uhalisia wa mazingira na mahitaji ya nchi na hapa Tanzania inatekelezwa na kusimamiwa na TFCG) tukiboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia pamoja na upatikanaji wa elimu bora shuleni kupitia mfumo wa elimu.

“ Tunafanya pia kazi ya   kuwajengea uwezo walimu na wafanyakazi wa wilaya ili kutoa elimu bora kuongeza uelewa na kuunga mkono haki za mtoto hususani za mtoto wa kike za kupata elimu bora,”amesema Meshack.

Mkuu wa Shule ya Msingi Kwelikwiji, Wilaya ya Mvomero, Evance Mwelondo amesema kupitia Programu ya Eco-School imewezesha shule hiyo kuanzisha miradi mbalimbali yenye mrengo wa kuhifadhi mazingira.

“Tuna miradi 13 ikiwemo ya kilimo cha iliki, vanilla, kokoa, ufugaji nyuki mizinga 26 ambapo shule imekuwa ikinufaika baada ya kuuza mazao na kupata fedha ambazo zinatatua changamoto mbalimbali,”amesema Mwelondo. 

Related Posts