Marehemu Ulomi alikuwa koplo wa Polisi

Dar es Salaam. Kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu Dodoma, Elisante Ulomi amesema mdogo wake, Daisle Simon Ulomi aliyefariki dunia kwa ajali ya pikipiki jijini hapa, alikuwa mtumishi wa Jeshi la Polisi kabla ya kuacha kazi hiyo mapema mwaka huu.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Ulomi aliyekuwa anafanya biashara ya fedha ya mitandao ya simu alipata ajali Desemba 11, 2024 majira ya 7:55 mchana maeneo ya Gereji External na kabla ya familia yake kuja kuutambua mwili wake Desemba 16, 2024 katika mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala.

Akizungumza leo Desemba 19 katika ibada ya kuaga mwili huo Kanisa la KKKT, Usharika wa Madale Betheli Dar es Salaam, Kamishna Ulomi amesema kifo chake kimekuwa cha ghafla amefariki akiwa na miaka 43.

“Alikuwa mtumishi wa Jeshi la Polisi kuanzia Mwaka 2006 hadi mapema mwaka huu akiwa na cheo cha Koplo.

“Kifo chake kimetuumiza kwani bado kama familia tulikuwa tunamuhitaji, mke wake alikuwa anamuhitaji na watoto wake walikuwa wanamuhutaji zaidi,” amesema.

Amesema baada ya kuacha kazi alikuwa anaendelea na majukumu mengine ikiwemo shughuli za kibiashara.

“Kifo chake ni pigo kwetu, lakini kwa kuwa ni mapenzi ya mwenyezi Mungu tuache tutaonana baadaye Mbinguni,” amesema.

Related Posts