Dar es Salaam. Jeshi la Polisi la Tanzania limetajwa kuwa miongoni mwa majeshi bora 10 barani Afrika kwa kuwa na weledi na kuheshimu haki za wananchi, utafiti wa Afrobarometer umebainisha.
Katika kigezo hicho, Burkina Faso imeongoza ikifuatiwa na Morocco, Niger, Benin, Mali, Senegal, Tanzania, Madagascar, Mauritania na Mauritius.
Mbali na kigezo hicho, pia Tanzania imeongoza kwa wananchi kuwa na imani na polisi, ikishika nafasi ya pili kwa wananchi kutohofia usalama wao.
Kwa matokeo hayo, Jeshi la Polisi Tanzania limeyapita majeshi ya nchi za Afrika Mashariki zikiwamo Kenya na Uganda ambazo kwa ujumla zimefanya vibaya katika vigezo mbalimbali vilivyotumiwa katika utafiti huo.
Hayo yamo kwenye ripoti inayoitwa “Watekelezaji Sheria au Wavunjaji Sheria?” iliyotolewa na taasisi ya Afrobarometer mapema mwaka huu iliyofanya uchambuzi kwa miaka mitatu kuanzia 2021 hadi 2023.
Utafiti huo wa awamu ya tisa umefanywa kwa mataifa 39 Afrika, ambapo Afrobarometer imewahoji watu 53,444 kwa lugha anayochagua mhojiwa na takwimu zimepimwa ili kuhakikisha sampuli zinawakilisha kitaifa.
Vigezo vilivyoangaliwa ni pamoja na uwepo wa polisi, utaalamu wa polisi: ufisadi na uhalifu wa polisi, ukatili, uhusiano kati ya vipengele vya utendaji wa polisi, matokeo yanayohusiana na mwenendo wa polisi.
Akizungumzia matokeo hayo, Mkurugenzi wa Utetezi na Mageuzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe, licha ya kupongeza jeshi hilo amesema si lazima vigezo hivyo viakisi hali halisi.
“Inawezekana wamefanya vizuri kutokana na vigezo na kutegemea ni wapi wametoa taarifa hizo, kwa sababu kumekuwa na matukio mengi ya uhalifu ambayo polisi wanatuhumiwa na mpaka wenyewe wamechukuliana hatua.
“Kwa mfano lile tukio la mauaji ya mfanyabiashara wa madini kule Mtwara ambalo polisi wameshtakiwa,” amesema.
Ameongeza kuwa kutokana na Tanzania kutosikika katika vyombo vya habari kimataifa, huenda hata sifa zake mbaya hazisikiki.
“Ni tofauti na Kenya ambayo inasikika zaidi kwenye vyombo vya kimataifa pengine ni kutokana na lugha ya Kiingereza,” amesema.
Pamoja na hayo, Massawe amelipongeza Jeshi la Polisi akishauri lifute rekodi mbaya zilizopo ili ziakisi sifa iliyotolewa na ripoti hiyo.
Maoni hayo yamekuja wakati hivi karibuni, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba alilikosoa Jeshi la Polisi akisema limejiingiza katika siasa, alipokuwa akitoa tathmini ya uchaguzi wa serikali za mitaa jijini Dar es Salaam.
“Polisi ni chombo muhimu sana, ndicho kinacholinda wananchi na mali zao na kinatakiwa kifanye kazi na wananchi wote, katika miaka michache iliyopita tumeliingiza Jeshi la Polisi katika siasa za nchi, linatoa matamko ya kisiasa na hii italeta mgawanyiko, wananchi watagawanyika,” alionya Jaji Warioba.
Alipotafutwa kuzungumzia utafiti huo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime hakupokea simu na hata alipotumiwa ujumbe hakujibu hadi tunachapisha taarifa hizi.
Mbali na kigenzo cha weledi na kuheshimu haki za wananchi, Tanzania imeongoza katika kigezo cha wananchi kuwa na imani na Jeshi la Polisi, ikiwa na asilimia 79 ukilinganisha na Uganda iliyoshika nafasi ya 27 na Kenya ya 30, Nigeria ikiwa ya mwisho.
Katika kigezo cha kutohofia usalama au kutoogopa uhalifu, Seychelles imeongoza (asilimia 80), ikifuatiwa na Tanzania (asilimia 75), huku Burkina Faso ikishika nafasi ya mwisho.
Katika kigezo cha jinsi Serikali inavyopunguza uhalifu, Tanzania nafasi ya pili (asilimia 74) nyuma ya Benin (asilimia 77), huku Sudan ikiwa ya mwisho.
Hata hivyo, Tanzania haijafanya vizuri katika kipengele cha uwepo wa polisi mijini na vijijini, ikishika nafasi ya 39 (asilimia 55 polisi mjini na asilimia 14 vijijini).
Nchi iliyoongoza katika kigezo hicho ni Morocco ikiwa na asilimia 94 ya polisi mijini na asilimia 31 vijijini.
Katika kigezo cha wananchi kuwasiliana na polisi, Tanzania imeshika nafasi ya 34 ikiwa na asilimia 9 ya watu walioomba msaada na asilimia 24 ya watu waliowasiliana na jeshi hilo kwa namna nyingine.
Katika kigezo cha wepesi wa kupata msaada wa polisi, Tanzania imeshika nafasi ya 11 ikiwa na asilimia 26 ya wepesi zaidi na asilimia 35 ya wepesi.
Katika kigezo cha ‘mara ngapi polisi husimamisha madereva bila sababu za msingi’, Tanzania imeshika nafasi ya 24 ikiwa na asilimia 37 ya mara kwa mara, asilimia 22 ya mara kadhaa na asilimia 35 ya mara chache au hakuna.
Katika kigezo hicho, Gabon imeongoza ikifuatiwa na Kenya. Kigezo cha wananchi kutoa rushwa ili kupata msaada wa polisi au kujiepusha na matatizo, Tanzania imeshika nafasi ya 26 ikiwa na asilimia 28 ya kutoa rushwa ili mtu asaidie na asilimia 28 ya kutoa rushwa ili mtu aachiwe.
Katika kundi hilo, Liberia inaongoza ikifuatiwa na Nigeria, Sierra Leone, Uganda na Congo- Brazzaville.
Katika taasisi zinazoongoza kwa rushwa, polisi imetajwa kuwa taasisi inayoongoza Afrika, ikifuatiwa na wabunge, maofisa wa kodi, watumishi wa umma, ofisi za marais, watendaji wa biashara, majaji na mahakama, serikali za mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa jadi na viongozi wa dini.
Katika taasisi hizo, polisi wa Uganda wanaongoza wakifuatiwa na Nigeria, Sierra Leone, Gabon, Kenya, Liberia, Ghana, Afrika Kusini, Cameroun na Msumbiji huku Tanzania ikishika nafasi ya 32.
Katika kigezo cha jinsi polisi wanavyohusishwa na uhalifu, Tanzania imeshika nafasi ya 38, ikiwa na asilimia 11 ya mara zote, asilimia 15 mara kadhaa, asilimia 13 hawajui na asilimia 61 walisema mara chache au hakuna kabisa.
Katika eneo hilo, Lesotho imeongoza, huku Kenya ikishika nafasi ya sita na Uganda nafasi ya 11.
Katika kigezo cha ukatili wa polisi, Tanzania imeshika nafasi ya 32, ikiwa na asilimia 28 mara kadhaa, asilimia 26 mara kadhaa na asilimia 6 wakisema hawajui huku asilimia 40 wakisema mara chache au hakuna kabisa.
Katika eneo hilo, Gabon imeongoza, Kenya ikishika nafasi ya tatu na Uganda ya nne.
Katika kigezo cha matumizi ya nguvu kubaini wahalifu, Tanzania imeshika nafasi ya 22, ambapo asilimia 42 wamesema wakati wote, asilimia 24 mara kadhaa na asilimia tatu hawajui na asilimia 31 wamesema mara chache au hakuna kabisa.
IGP na hali ya usalama nchini
Septemba 12, 2024 Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillus Wambura wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa Mwaka wa Maofisa wakuu waandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, alisema hali ya usalama nchini ni shwari kutokana na kazi nzuri inayofanywa na jehi hilo.
Wambura alisema jeshi hilo limejiimarisha zaidi katika mikakati ya kuzuia uhalifu ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa kuwashughulikia wahalifu.
Kilio cha utekaji, mauaji ya raia
Licha ya mazuri hayo, hivi karibuni Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Maimu, alisema masuala ya utekaji na mauaji yanayotokea nchini yanatakiwa kufanyiwa kazi kwa kina, ili kuondokana nayo kwa sababu yanaiharibia nchi.
Jaji Maimu alitoa kauli hiyo wakati kukiwa na mfululizo wa matukio ya watu kudaiwa kutekwa na wengine kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.
Hata hivyo, tayari Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa ameyakemea na kuagiza uchunguzi wa kina ufanyike na taarifa apelekewe.
Baadhi ya matukio ya hivi karibuni ni lile la Desemba 1, 2024 la Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT- Wazalendo, Abdul Nondo kuchukuliwa na watu wasojulikana.
Nondo alichukuliwa alfajiri katika Kituo cha mabasi cha Magufuli, Dar es Salaam akitokea Kigoma kwenye shughuli za kisiasa. Jeshi la Polisi likasema linafuatilia kwani alichukuliwa na watu wasiojulikana wakiwa na gari aina ya Land Cruiser.
Siku hiyo hiyo usiku, Nondo alitelekezwa Coco Beach kisha yeye akaomba msaada wa bodaboda wakampeleka makao makuu ya chama chake, Magomeni na baadaye kutibiwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Tukio lingine ni la Desemba 3, 2024 la Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Tawi la Machinjioni, Kata ya Makongorosi Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya, Michael Kalinga kukutwa ameuawa na mwili wake kutelekezwa.
Tukio jingie ni lile la kupigwa risasi hadi kufariki dunia kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Christina Kibiki Novemba 13, 2024. Tayari watu watatu wanashikiliwa na polisi.