Mgunda alivyowaficha mastaa wa Azam FC

UWEPO wa Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin katika eneo la kiungo cha Simba kuiwapa wakati mgumu Azam FC ambayo ilikumbana na kipigo cha mabao 3-0 jana, Alhamisi, katika mchezo wa vita ya kuwania kumaliza msimu kwenye nafasi mbili za juu katika Ligi Kuu Bara.

Kabla ya mchezo huo ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa huku idadi ya mashabiki ikionekana ndogo, Simba ilikuwa nyuma ya Azam FC kwa tofauti ya pointi nne, hivyo ushindi huo umeifanya kufikisha 56 na hivyo kuwa nyuma kwa pointi moja, huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi.

Viungo hao walimudu kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja huku wakibadilishana nafasi, walizuia wakati wakishambuliwa kwa muundo wa pembe tatu na kupandisha mashambulizi kwa kupiga pasi ndefu katika mianya ambayo Azam ilikuwa ikiiacha.

Azam ambayo ilikuwa bora katika kipindi cha kwanza ilikuwa ikitumia maeneo yake ya pembeni kupandisha mashambulizi kutokana na kasi ya washambuliaji wake, Gibril Sillah na Idd Seleman ‘Nado’ huku mabeki wao wa pembeni, Nathaniel Chilambo na Pascal Msindo wakisogea juu.

Katika namna hiyo ya uchezaji, Simba nayo ilitumia kasi ya wachezaji wake wa pembeni, Edwin Balua na Ladack Chasambi huku viungo wake wa kati wakiwa na jukumu moja tu la kupiga mipira mirefu katika mianya ambayo wachezaji wa Azam walitoka wakati wakisogea kushambulia.

Muda mwingine alionekana Mzamiru kutokana na kasi aliyonayo akipanda na mipira ili kuongeza idadi ya namba ya wachezaji katika kushambulia jambo ambalo lilionekana kuwa na matunda katika kipindi cha pili ambacho Simba ilionekana kuwa bora zaidi.

Namna ambavyo viungo hao walikuwa wakicheza waliwapa wakati mgumu, James Akaminko na Yahya Zayd ambao walikuwa wakicheza mbele ya mabeki wao wa kati, Yannick Bangala na Mcolombia Yeison Fuentes.

Kutokana na hali hiyo kocha wa Azam, Youssouph Dabo alifanya mabadiliko kadhaa katika eneo hilo ambayo hata hivyo hayakuzaa matunda kutokana na mpango mzuri ambao Mgunda aliingia nao.

Katika mchezo huo wa maamuzi, Azam ilipoteza nafasi ya kuwa mbele katika kipindi cha kwanza baada ya Sillah kuangushwa na Che Malone aliyekuwa katika harakati za kuzuia katika eneo la hatari.

Hata hivyo mkwaju wa Feisal Salum aliyekuwa na shauku ya kufunga bao lake la 16 msimu huu, uligonga nguzo na kuufanya timu hizo kwenda mapumziko wakiwa suluhu kabla ya kibao kuwageukia kipindi cha pili na kuruhusu mabao matatu katika dakika ya waliyofungwa na Kanoute, Ngoma na David Kameta ‘Duchu’.

Mbali na nafasi hiyo mwanzoni mwa mchezo huo, Azam ilipoteza nafasi ya wazi baada ya beki wa kulia wa Simba, Israel Mwenda ‘kuchoma’ kwa  kupiga pasi fupi ambayo ilinaswa na almanusura Sillah afunge lakini alimalizia vibaya na mpira ukagonga nguzo.

Mara kadhaa katika kipindi hicho cha kwanza, kipa wa Simba, Ayoub Lakred naye alikuwa kikwazo cha vijana hao wa Dado.

Mara baada ya mchezo huo mashabiki wachache wa Simba ambao walijitokeza kwenye uwanja wa Mkapa, walikuwa wakiliimba jina la Mgunda kwa kudai ‘anatosha’ kutokana na kuisaidia kuvuna pointi 10, huku ikionekana kutandaza kandanda la kuvutia.

Mgunda alianza majukumu ya kukaimu nafasi ya Abdelhak Benchikha Ruangwa, Lingi  ambako alivuna pointi moja kwa kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Namungo na baada ya hapo ameingoza Simba kushinda michezo mitatu mfululizo bila ya kuruhusu bao.

Michezo hiyo ni dhidi ya Mtibwa Sugar (2-0), Tabora United (2-0) na Azam FC (3-0).

Akizungumzia mwenendo wa kikosi na ushindi ambao wameupata dhidi ya Azam FC, Mgunda amesema: “Tuliwapa majukumu na kila mmoja ameyafanya kwa nafasi yake, hili limeisha bado tuna mchezo mwingine mgumu mbele yetu (wa Kagera Sugar) ambao tunatakiwa kushinda.”

“Azam ilikuwa bora lakini tulijua udhaifu wao, hivyo tulijiandaa huku tukijua aina ya mpinzani ambaye tutakabiliana naye.”

Kitendo cha Simba kupunguza tofauti ya pointi na kusalia moja baina yake na Azam  kimeifanya kuweka hai matumaini ya kumaliza msimu katika nafasi mbili za juu, huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi.

Kama Simba yenye pointi 56 itaibuka na ushindi Jumapili dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Katiba, Bukoba, itaishusha Azam yenye pointi 57 katika nafasi ya pili huku ikisalia michezo minne kila upande.

Baada ya kumalizana na Kagera Sugar, Simba itakuwa na kibarua cha kusaka pointi 12 dhidi ya Dodoma Jiji, Geita Gold, KMC na Maafande wa JKT Tanzania. Kwa upande wa Azam FC mechi nne zilizosalia ni dhidi ya KMC, JKT Tanzania, Kagera Sugar na Geita Gold.

Related Posts

en English sw Swahili