Yanga pamechangamka huko… Pacome, Yao kama utani

YANGA jana ilikuwa uwanjani kumalizana na Mashujaa ya Kigoma katika Ligi Kuu Bara, lakini kuna jambo moja limefanyika kimya kimya ambalo kama taarifa hii itawafikia mashabiki wa klabu hiyo itawapa mzuka juu ya mastaa wawili wa timu hiyo, kiungo mshambuliaji Pacome Zouzoua na beki wa kulia Yao Kouassi.

Nyota hao ambao Mwanaspoti liliwahi kuwahabarisha kuwa mikataba yao na klabu ya Yanga ipo mwishoni na kulikuwa na mazungumzo yanayoyoendelea chini kwa chini ili kutaka kuongezewa mipya, hata hivyo kulielezwa kuna kaugumu flani kwa Pacome, lakini kwa sasa ni kwamba wawili hao wamemaliza utata na watakuwapo sana.

Ipo hivi. Mabosi wa Yanga wameshusha presha za mashabiki na wapenzi wa Yanga kwa kufanikiwa kuwabakisha kikosini nyota hao wawili raia wa Ivory Coast, baada ya kuwasainisha mikataba mipya na muda wowote kuanzia sasa watatambilulishwa rasmi kuonyesha kuwa wote ni mali ya Wananchi kwa miaka mingine miwili kila mmoja.

Pacome ambaye msimu wa kwanza tu alifanya kazi kubwa akifunga mabao saba na msimu huu kuongeza mengine matatu na asisti mbili hadi sasa, mbali na yale ya michuano ya kimataifa, alikuwa akiziweka roho za mashabiki wa Yanga baada ya kudaiwa alikuwa kama anadengua flani kuongeza mkataba mpya, huku Simba ikitajwa kummezea.

Hata hivyo, vigogo wa Yanga walifanya kweli kwa kuzungumza naye na kukubaliana kuongeza mkataba mpya wa miaka miwili, huku kiwango kikubwa alichonacho kikimpa nafasi kwa makocha wote wawili waliomnoa kuanzia Miguel Gamondi aliyeondolewa hivi karibuni na sasa Sead Ramovic kutumika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Mbali na Simba, Pacome alikuwa akihusishwa pia na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na Azam zilizokuwa zikimpigia hesabu za kumbeba wakati alipokuwa akidengua kusaini mkataba huo mapema hata kabla ya Gamondi hajaondoka na kuacha ripoti kwamba ni lazima asalie kikosini kutokana na umuhimu wake.

Taarifa za ndani ya Yanga zinasema, Pacome na Yanga mambo yamekaa sawa na kilichobaki ni kutangazwa hadharani kuwa ataendelea kuwepo Jangwani kwa miaka miwili ijayo, kama ilivyo kwa beki wa kulia, Yao Kouassi ambaye naye mkataba wake wa awali ulikuwa ukingoni.

Yao aliyeasisti saba akizidiwa mbili na aliyekuwa kinara wa msimu uliopita, winga wa Azam Kipre Junior aliyemaliza na tisa, alitua Yanga misimu miwili iliyopita akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast kama Pacome na hata Stephane Aziz KI aliyewatangulia kwa msimu mmoja zaidi.

Licha ya msimu huu Yao kutokuwa na makali kama ya msimu wa kwanza, ikielezwa ni kutokana na majeraha aliyokutana nayo hivi karibuni, lakini hiyo haikuwazuia mabosi wa Yanga kumpa mkataba mpya ili aendelee kuwepo kikosini kutokana na ubora alionao wa kulinda, kuanzisha mashambulizi na kuasisti.

Hata hivyo, katika kukabiliana na majeraha aliyonayo, Yanga iliamua kumleta Yao beki mzawa Israel Mwenda anayeungana na Kibwana Shomari kuwania nao namba.

“Tusingeweza kufanya makosa ya kuwaacha au kuruhusu wachezaji hawa kuondoka, kila mmoja ameshasaini mkataba wa miaka miwili kubaki hapa,”alisema bosi huyo wa juu wa Yanga.

Meneja wa wachezaji hao Zambro Traore, japo hakutaka kueleza kwa kirefu ameliambia Mwanaspoti kuwa Pacome na Yao wataendelea kusalia zaidi ndani ya klabu hiyo.

“Pacome na Yao ni wachezaji ambao wanaendelea vizuri kutumikia mikataba yao na wameamua kuendelea zaidi kubaki hapo hata baada ya msimu huu kumalizika, kama unavyoona wana furaha na klabu yao,” alisema Traore.

Hii si mara ya kwanza kwa Yanga kuongeza mkataba kwa mastaa wanaofanya vizuri, kwani msimu uliopita walimuongezea Aziz KI baada ya awali kuwepo kwa presha za kutakiwa na klabu kadhaa zilizopo Afrika, na mwamba huyo alifanya yake akimaliza kama kinara wa mabao akifunga 21 na asisti saba akiipa Yanga ubingwa.

Related Posts