Dar es Salaam. Utoaji elimu bila malipo inatajwa kuwa moja ya sababu ya kuwapo ongezeko kubwa la wanafunzi linaloshuhudiwa kila mwaka katika shule mbalimbali nchini.
Wilaya ya Temeke ni miongoni mwa zile zilizoathiriwa na hali hiyo na kufanya baadhi ya shule kuwa na wanafunzi wengi kuliko uwezo wake.
Mbali na elimu bila malipo, pia ukuaji wa miji na kuzaliana ni sababu nyingine zinazotajwa kuchangia kuwapo kwa ongezeko la wanafunzi.
Akizungumza na Mwananchi, mtafiti wa uchumi, Muhanyi Nkoronko anasema sera ya elimu bila malipo imefanya wanafunzi kuongezeka, hali iliyofanya madarasa kuwa machache na walimu kutotosheleza.
“Kukiwa na mrundikano kuna athari katika ufundishaji na ujifunzaji, mwalimu hawezi kumfikia mwanafunzi mmoja mmoja, wanafunzi watakaofikiwa ni wale walio mbele au wanaoonyesha maendeleo fulani,” anasema Muhanyi.
Anasema hali hiyo inafanya ujifunzaji kuwa hafifu na wanafunzi wanashindwa kupata maarifa inavyotakiwa. Pia mzigo kwa mwalimu katika kuandaa masomo anayoweza kuwafundisha wanafunzi inakuwa ngumu na anashindwa kufanya tathmini kujua kama wanafunzi wake wanaelewa.
Hiyo inatokana na kushindwa kusahihisha kwa wakati au kushindwa kutoa mazoezi ya upimaji yanayoendana na kile anachofundisha.
“Hali hii inamfanya kutoa mazoezi rahisi katika kusahihisha kama ni kuchagua basi, hii haimpimi vyema wanafunzi na kama mwalimu anashindwa kuwapa huduma stahiki,” anasema Nkoronko.
Anasema athari yake ni kuwa wanafunzi wanamaliza bila kuwa na maarifa wanayoweza kutumia katika maisha ya kila siku au maarifa yatakayowawezesha kufaulu kuendelea katika hatua inayofuata.
Mbali na elimu bila malipo, kuzaliana ni miongoni mwa mmbo yanayoipa tabu wilaya hiyo na limewahi kuzungumzwa hadi bungeni jijini Dodoma.
Mei 5, 2021, Mbunge wa Temeke (CCM), Dorothy Kilave aliihoji Serikali ina mpango gani wa kujenga shule katika jimbo la Temeke kwa sababu wana watoto wengi wa darasa la kwanza, akidai wanatokana na wananchi wa eneo hilo kuzaliana sana.
Katika ukuaji wa miji, Mkuu wa Wilaya wa Temeke, Sixtus Mapunda anasema maisha ya Kinondoni na Ilala ni magumu, jambo linalofanya watu kukimbilia wilayani kwake kutafuta urahisi wa maisha, jambo linalofanya eneo hilo kuendelea kuelemewa na idadi ya watu.
Pia kuimarika kwa miundombinu na uwepo wa magari yanayokwenda sehemu zote, yameweka urahisi kwa watu kusafiri kutoka upande mmoja kwenda mwingine, jambo linalowafanya kuona urahisi wa kukaa sehemu hiyo. Wilaya hiyo kuwa karibu na mikoa ya kusini pia ni sababu nyingine ya shule zake kuelemewa na wanafunzi, kwani wageni wengi kutoka mikoa hiyo wengi ndiyo mwisho wao wa safari.
Kuhusu kuzaliana nayo aliitaja, huku akitolea mfano wa watoto wanaopewa vyeti vya kuzaliwa.
Kwa mujibu wa maelezo yake, kati ya Agosti hadi Oktoba mwaka huu, wastani wa vyeti 2,000 hadi 2,500 vilitolewa, huku akiweka bayana hiyo ni ishara ya kuwa wanaozaliwa ni zaidi ya hao.
“Unaweza kusema wanaozaliwa ni zaidi ya 5,000, kwani hawa tunaowasajili ni wale wanaojua umuhimu wa vyeti vya kuzaliwa. Sasa unaweza kuona ongezeko hili, ardhi iliyopo iko vilevile, ila watu wanaongezeka,” anasema.
Hali hiyo imefanya shule kuelemewa na idadi ya wanafunzi, huku akitolea mfano wa Shule ya Msingi Chamazi, ambayo baadhi ya wanafunzi wanalazimika kukaa nje.
Hiyo imeathiri hata idadi ya wanafunzi kwa darasa, kwa kile anachokisema mkuu wa wilaya, kwani hata makadirio ya wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza yanayofanywa ili kuandaa miundombinu yamekuwa tofauti na hali halisi.
“Mfano, mwaka jana tulifanya makadirio watakaojiunga kidato cha kwanza watakuwa kati ya 13,000 hadi 15,000 lakini waliojiunga walikuwa 26,000, unaweza kuona ni asilimia ngapi ya tuliokuwa tumetarajia, wanaingia wengi kuliko waliotoka kwa sababu ya elimu bila malipo,” anasema Mapunda.
Maneno yake hayatofautiani na Ofisa Mipango wa wilaya ya Temeke, Shafi Kipande anayesema ukuaji wa miji ni moja ya changamoto inayofanya baadhi ya shule kuonekana kuelemewa na wanafunzi.
Akitolea mfano Mbagala, anasema eneo hilo ni miongoni mwa sehemu zinazojengwa na watu kuhamia sana na katika baadhi ya maeneo bado miundombinu ya shule haijajengwa, hivyo kufanya watu wote kutegemea zile zilizopo.
“Watoto nao wanazaliwa wengi, jambo linalofanya miji kukua, pia hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule, jambo ambalo linahitaji fedha za fidia kila unapohitaji kujenga shule,” anasema Kipande.
Suala lingine ni kutokuwapo kwa uwiano kati ya wanafunzi wanaomaliza shule na wanaoanza, jambo linalofanya miundombinu kuelemewa, huku akitolea mfano wa wanafunzi 700 kumaliza na kusajiliwa 1,000.
“Kitu kingine ni watu kufuata shule baada ya kusikia inafanya vizuri, kwa hiyo anakuwa tayari kumtoa mtoto wake mbali ili asome shule hiyo,” anasema.
Namna ya kushughulika nalo
Mrundikano wa wanafunzi kwa darasa katika baadhi ya shule nchini ni jambo linalopaswa kusimamiwa kwa ukaribu na Serikali, ikiwemo wathibiti ubora.
Katika kushughulika na hilo, mdau wa elimu, Muhanyi Nkoronko anasema ni vema Serikali iongeze kiwango cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya kuhudumia utoaji wa elimu msingi. “Fedha hizi zitasaidia kuajiri walimu wengi na kujenga miundombinu ya madarasa, kama tutaongeza uwekezaji vitu kama hivi hatuwezi kuvisikia,” anasema Nkoronko.
Anasema katika ujenzi wa madarasa zipo namna mbili ambapo ya kwanza ni halmashauri husika kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule, ikiwemo madarasa, huku namna nyingine ikiwa ni kuwashirikisha wazazi wachangie fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu.
Mmoja wa walimu wakuu wa shule ambazo Mwananchi ilifanyia uchunguzi aliitaka Serikali kuangalia namna inavyoweza kufanya ujenzi wa shule nyingine mpya, ili kupunguza idadi ya wanafunzi waliopo katika shule yake kwa kile alichokisema shule yake inaweza kuzaa nyingine mbili.
“Idadi niliyonayo naweza kutoa shule nyingine mbili zilizojaa wanafunzi, watoto wakiwa wengi hivi hata wengine wanaweza kuacha shule usijue,” anasema mwalimu huyo.
Anachokisema mwalimu huyo kiliwahi kufanywa kwa miaka tofauti ambapo shule mpya, ikiwemo ya Mbande Kisewe ilizaliwa kutoka shule ya msingi Mbande.
Katika kuendelea kushughulika na suala hilo, Kipande aliliambia Mwananchi kuwa wapo katika hatua za kufanya ujenzi wa shule nyingine mbili mpya ambazo zitasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Shule hizo zilizopewa majina ya Moringe na Dovya, kila moja itakuwa na madarasa saba ya msingi, mawili ya awali, matundu 10 ya vyoo, majengo ya utawala na sehemu za kuchomea taka.
“Shule hizi kila moja itagharimu Sh309.9 milioni, zitatumia ‘force account’ katika ujenzi wake na matarajio yetu ni Januari mwakani zianze ujenzi,” anasema.
Hata hivyo, bado haijajulikana shule hizo zitajengwa katika maeneo gani, kutokana na Serikali kukosa maeneo yaliyoainishwa kwa ajili ya huduma za kijamii, hivyo kila jambo linapotaka kufanyika fidia inahitajika kulipwa kwa wananchi watakaopisha mradi huo. Anasema wingi huo wa wanafunzi umeifanya Temeke sasa kuangalia namna ya kurekebisha madarasa yaliyopo na kuongeza mengine kwenda juu, huku akiweka bayana kuwa ili kumaliza tatizo hilo mpango wa muda mrefu unahitajika, kwa sababu mara zote idadi ya wanafunzi wanaojiunga masomo hawatabiriki ikilinganishwa wanaomaliza shule.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.