KenGold yashusha majembe | Mwanaspoti

KICHAPO cha mabao 2-0, ilichokipata KenGold juzi dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kimezidi kuwaamsha mabosi wa timu hiyo, ambayo kwa sasa inapambana kukinasua mkiani baada ya kufukuzia saini ya mshambuliaji Mghana, Eric Okutu.

KenGold inayoburuza mkiani mwa msimamo na pointi zake sita baada ya kucheza michezo 15, ikishinda mmoja, sare mitatu na kupoteza 11, tayari mabosi wa timu hiyo wanaangalia uwezekano wa kumpata Okutu kwa mkopo akitokea Pamba Jiji ya Mwanza.

Nyota huyo amejiunga na timu hiyo msimu huu baada ya kuachana na Tabora United aliyojiunga nayo mara ya kwanza msimu wa 2023-2024 akitoka Hearts of Lions ya Ghana na akiwa na kikosi hicho cha Nyuki wa Tabora, alikifungia mabao saba ya Ligi.

Taarifa kutoka ndani ya KenGold zimeliambia Mwanaspoti juzi mabosi hao walikuwa na mazungumzo ya kumpata nyota huyo kwa mkopo wa miezi sita, huku dili hilo likikaribia kukamilika baada ya Pamba kumsajili Mkenya, Mathew Tegisi Momanyi kutoka Shabana FC.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba, Ezekiel Ntibikeha alisema maboresho yoyote yatakayotokea ndani ya kikosi hicho watayaweka wazi, kama walivyoanza kutangaza usajili wa mastaa wapya waliowasajili dirisha hili.

“Tumeanza na utaratibu wa kutangaza usajili wa nyota wapya watakaoongezea nguvu kikosi chetu na ikifika muda pia wa kutangaza tulioachana nao tutafanya hivyo, tunaendelea kufanyia tathimini kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi.”

Kwa upande wa Okutu alisema hadi sasa hana taarifa zozote ingawa kama itatokea ataweka wazi, japo malengo yake ni kuhakikisha anaendelea kupigania nafasi na washambuliaji waliopo Pamba.

Mbali na nyota huyo KenGold iko katika hatua za mwisho za kukamilisha saini za Sadala Lipangile kutoka Biashara United, Stephen Sey ambaye kwa sasa yuko huru baada ya kuachana na Anwar Al-Abyar ya Libya na Obrey Chirwa kutoka Kagera Sugar.

Wengine ni beki wa kati, Sandale Komanje aliyekuwa anaichezea Tabora United na kiungo mshambuliaji, Lassa Kiala ambaye yupo huru, baada ya kuzichezea timu za FC Saint Eloi Lupopo ya kwao DR Congo, Kitwe United na Zanaco FC zote za Zambia.

Related Posts