AKILI ZA KIJIWENI: Wachungaji wajiandae kupokea wachezaji

KILICHOTOKEA katika siku hizi za karibuni kinaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kubadilisha mitazamo na fikra za wachezaji wetu.

Na hivi ndivyo hapa kijiweni tunapenda kuona kwamba wachezaji wawe wanajifunza mara kwa mara na kuwa na mawazo chanya.

Jambo lenyewe ni wachezaji wawili wa nafasi ya mshambualiaji wa kati wa timu kongwe nchini za Yanga na Simba kwenda kwa wachungaji kuombewa kisha siku chache baadaye wakazifungia mabao timu zao.

Ilianzia kwa Prince Dube wa Yanga, ambaye baada ya kusota kwa muda mrefu bila kufumania nyavu, alipachika bao la kusawazisha katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ugenini huko DR Congo, na jana alifunga hat trick kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa.

Picha mbalimbali zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zinamuonyesha Dube akiombewa na mmoja wa wachungaji na siku chache baadaye akamaliza ukame wa mabao kwa kufunga dhidi ya Mazembe.

Baadaye mshambuliaji Leonel Ateba wa Simba naye akafunga mabao mawili katika mechi moja kwa mara ya kwanza tangu alipojiunga na timu hiyo huku pia akimaliza ukame wa kutofunga bao katika mechi tatu mfululizo.

Kumbe Ateba naye kabla ya mechi hiyo, alienda kwa mtumishi wa Mungu kupigwa maombi ili nuksi ya kutofunga iishe na kweli buana akatupia mabao mawili dhidi ya Kengold.

Ni jambo la kufurahisha kuona sasa wachezaji wanaona bora wajikabidhishe kwa Mungu pindi mambo ya uwanjani yanapokuwa hayawaendei sawa badala ya kukimbilia kwa masangoma.

Inavyoonekana baada ya mambo kuwanyookea Dube na Ateba, kuna kundi kubwa la wachezaji litaanza kukimbilia kwa wachungaji na mashehe kwenda kuombewa. Ni vyema kwenda kuomba Mungu badala ya kwenda kwa waganga wa kienyeji.

Related Posts