PEP kingatiba dhidi ya VVU iko hivi

Kitabibu PEP ni kifupisho cha Post Proplaxis Exposure, ni mwongozo wa matibabu kwa kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi, ARVs kama kingatiba dhidi ya virusi vinavyosababisha Ukimwi.

Zinatumika mara baada ya kuingia katika hatari kubwa ya maambukizi ya VVU. Neno “prophylaxis” kitabibu linamaanisha kuzuia kuenea kwa maambukizi au ugonjwa kwa kutumia dawa kama kingatiba.

Inapotumika kwa usahihi huweza kuzuia kwa zaidi ya asilimia 80% endapo itatumika ndani ya saa 72, yaani siku 3 baada ya uwezekano wa kuambukizwa VVU.

Kawaida muongozo wa PEP uliorithiwa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) huwa na dawa aina 2-3, zikiwa ni muunganiko wa kidonge kimoja ambazo hutumika mara 1 kwa siku kwa muda wa siku 28.

Kidonge kimoja huwa na dawa za ARVs, ikiwamo Tenofovir Disoproxil/Emtricitabine ambayo pia inajulikana kama Truvada na tembe mbili za Raltegravir.

PEP inaweza kutumiwa kwa watu wazima, vijana na watoto wenye tishio la kuambukizwa VVU wakati walipojamiiana, waliobakwa au wamenyanyaswa kingono na watumiaji wa madawa ya kulevya waliojidunga kwa kushirikiana sindano.

Vilevile wahudumu wa afya waliojijeruhi kazini wakati wa kuhudumia wagonjwa.

Ukiacha PEP, ipo PrEP ambacho ni kifupisho cha Pre Proplaxis Exposure. Hii yenyewe inalenga kuzuia VVU kabla ya kukaribia maambukizi.

Mfano wahudumu wa sehemu za burudani na wanaofanya biashara ya ngono. Makundi haya yako katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU, hunywa PREP kila siku au sindano kila baada ya miezi miwili.

Tukirudi kwa kingatiba PEP, inapaswa kutumika katika hali za dharura tu, haishauriwi kutumiwa mara kwa mara. Hii ni kwa sababu dawa hizo zina madhara machache kwa baadhi ya watumiaji, ingawa yanaweza kutibiwa na siyo hatari kwa maisha.

Toa taarifa mapema kwa mtoa huduma za afya kama una madhara yoyote yanayokusumbua au ambayo hayataisha.

Madhara hayo ni pamoja na kichefuchefu, mshtuko wa tumbo, uchovu na maumivu ya kichwa. Dalili hizi mara nyingi huisha baada ya wiki ya kwanza ya kutumia PEP.

Ili kuzuia hali ya kichefuchefu, chukua PEP pamoja na vitafunio au tumia kabla ya kulala ili kuipoteza hali hiyo. Unaweza pia kujaribu pipi zenye ladha za matunda.

Kwa kuwa faida ya kuitumia PEP kama kingatiba huwa ni kubwa zaidi kuliko madhara machache ya kuitumia, ndiyo maana inatumika kama dharura.

PEP haikukusudiwa kuchukua nafasi ya matumizi ya mara kwa mara ya njia nyingine za kuzuia VVU, ikiwamo matumizi sahihi ya kondomu wakati wa kujamiiana au kingatiba kabla ya kukaribia maambukizi, yaani PrEP.

Kwa mhudumu wa afya ambaye ana uwezekano wa kuambukizwa VVU, anapaswa kutafuta matibabu mara moja PEP kwa kuzingatia muongozo wa nchi husika.

Ufanisi wa PEP unategemea na mhusika kuweza kushikamana na mwongozo wa dozi ya PEP aliyoandikiwa na daktari, ikiwamo kumeza kidonge hicho kwa muda wa siku 28 kama ilivyoelekezwa.

Huhitaji PEP kama unatumia kondomu kwa ufanisi au unatumia PrEP au ikiwa mwenza wake yuko katika dawa za ARVs na ana kiwango kisichoonekana cha VVU.

Wakati wa kutumia PEP, ni muhimu kuendelea kutumia njia nyingine za kuzuia VVU, ikiwamo kutojamiiana na ukishindwa tumia kondomu. Tutumia sindano mpya tu wakati wa kujidunga dawa.

Iwapo utaingia katika hatari kubwa ya kuweza kupata VVU hivi karibuni, toa taarifa haraka kabla ya saa 72 kupita.

Related Posts