Mchungaji aliyemuua mkewe afungwa jela miaka 12

Uganda. Mahakama Kuu ya Luweero nchini Uganda imemhukumu kifungo cha miaka 12 jela Mchungaji wa Kanisa la Anglikana, David Ssekibaala baada ya kukiri kumuua mkewe, Deborah Ssekibaala, miaka minne iliyopita.

Hukumu hiyo imeweka tamati ya maswali yaliyokuwa yakiibuliwa kuhusu kifo cha Deborah kilichotokea usiku wa Novemba 9, 2020.

Desemba 11, akiwa mbele ya Jaji wa mahakama hiyo, Henrientta Wolayo, mchungaji huyo alikiri kutenda kosa la mauaji na kuomba msamaha kwa familia yake na umma kwa ujumla.

Jaji Wolayo amesema kukiri kosa bila kupoteza muda wa mahakama na kuonyesha kujutia ndiko kulikomfanya amuhukumu kifungo cha miaka 12 badala ya adhabu kali zaidi.

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani na Wakili Mkuu wa Serikali, Peace Bashabe mtuhumiwa alifanya mauaji hayo nyumbani kwake katika eneo la Kavule, Halmashauri ya Mji wa Luweero.

Tangu mauaji hayo, amekuwa akishikiliwa katika Gereza la Serikali la Nakasongola.

Siku ya tukio, wakazi wa Kavule walishtushwa na habari za kifo cha Deborah, ambaye mwili wake ulikutwa na majeraha ya moto ndani ya chumba kimojawapo cha nyumba wanayoishi.

Awali, Mchungaji Ssekibaala alidai mkewe alipigwa na bomu, lakini baadaye alibadili maelezo akisema Deborah alijichoma kwa kutumia petroli.

Polisi walipofika eneo la tukio, walikuta dumu la mafuta ya petroli ndani ya nyumba hiyo na uchunguzi ulibaini mwanamama huyo alifariki kwa kukabwa shingo kabla ya mwili wake kuchomwa moto, kitendo kilichoonekana kuwa jaribio la kuficha ushahidi.

Msamaha kutoka kwa familia

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, watoto wa Mchungaji Ssekibaala walipata nafasi ya kutoa maoni yao mahakamani.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa watoto wa mchungaji huyo alisema, “tumemsamehe baba yetu kwa kile alichofanya.”

Watoto hao walisema wameshampokea Kristo kama mwokozi wao na ndiyo iliyowafanya wawe tayari kumsamehe baba yao.

Rekodi za Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Luweero zinaonyesha kabla ya mauaji, Mchungaji Ssekibaala alihudumu kama mchungaji wa shule ya sekondari ya Buzibwera, chini ya Jimbo la Kikyusa.

Hata hivyo, aliondoka kwenye majukumu yake ya uchungaji kwa zaidi ya miaka mitatu kabla ya tukio la mauaji.

Askofu Mstaafu Eridard Kironde alisema wakati wa mauaji, Ssekibaala hakuwa tena sehemu ya viongozi wa kanisa la dayosisi hiyo.

Baadhi ya majirani walifichua kuwa, Ssekibaala alianzisha baa nyumbani kwake na alikuwa akiuza pombe huku pia akinywa.

Deborah, aliyekuwa mwanachama wa Umoja wa Wanawake wa Kanisa (Mothers’ Union) katika Dayosisi ya Luweero, alisimulia mara kadhaa kwa wanachama wenzake kuhusu unyanyasaji wa mumewe dhidi yake, jambo lililosababisha waumini kujaribu kuingilia kati.

Ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu iliyotolewa na polisi ilibainisha kuwa, licha ya mwili wa Deborah kuwa na majeraha ya moto, mifupa ya shingo yake ilivunjika.

Ripoti hiyo ilihitimisha kuwa Deborah alikabwa shingo hadi kufa kabla ya mwili wake kuchomwa moto, huku baadhi ya sehemu za mwili zikiwa hazikuungua, jambo lililothibitisha moto huo haukuwa chanzo cha kifo chake.

Chanzo: Daily Monitor- Uganda

Related Posts