Dar es Salaam. Wakati mwili wa John Tendwa aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ukizikwa leo Desemba 20, 2024, Padri wa Kanisa Katoliki Mbweni, Paulo Malewa ameeleza namna msajili huyo alivyoagana na familia yake saa chache kabla ya kifo chake.
Amesema siku kadhaa kabla ya kifo, Tendwa, aliomba aitiwe padri.
“Nilikwenda kuzungumza naye, alitaka ajipatanishe na Mungu na familia yake,” amesema Padri Malewa wakati wa ibada ya kuaga mwili wa Tendwa, iliyofanyika leo katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Vicent, Kibamba.
Amesema, Tendwa alitaka kufanya upatanisho na Mungu na familia yake.
“Alichoniambia siku hiyo sikisemi, lakini alitaka kufanya upatanisho na Mungu na familia yake,” amesema padri huyo.
Tendwa alifariki Desemba 17, 2024 alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa MuhimbilI (MNH).
Akizungumzia dakika za mwisho za Tendwa, Padri huyo amesema siku mbili kabla ya kifo chake Tendwa aliomba tena aitiwe Padri.
“Nilipigiwa simu Jumapili iliyopita (Desemba 15), nikaambiwa mzee (Tendwa) anataka kuzungumza na wewe, nikawambia msiwe wajinga, kama anamhitaji padri, muiteni padri yeyote lakini na mimi nakuja.
“Nilikwenda, nilipofika nikakuta anasema sema maneno, sikumjibu kitu, niliposali naye alisema padri nina furaha sana leo, akairudia kauli yake hiyo.
“Kisha akasema, ‘watoto wangu sasa ninakufa’. Tulikuwa na watoto wake pale, niliona hilo na Tendwa aliijua saa yake, baada ya saa chache hakuzungumza tena,” amesema Padri Malewa.
Amewambia waombolezaji inawezekana wanaijua historia na habari za Tendwa, lakini maisha yake ya mwisho Mungu alimwambia, “Mwanangu usife kama kondoo, alijipatanisha na Mungu na familia yake,” amesema padri huyo.
Mwili wa Tendwa uliagwa jana kitaifa, tukio lililoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.
Leo katika ibada hiyo, alikuwepo mwakilishi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ally Ahmed ambaye ni naibu msajili.
Tendwa alikuwa msajili wa vyama vya siasa kuanzia Mei 2001 hadi Agosti 2013 alipokabidhi kijiti kwa Jaji Francis Mutungi anayehudumu hadi sasa.
Hadi kifo chake, Tendwa alikuwa mshauri wa sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) katika masuala ya siasa na uchaguzi, pia alikuwa mwanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Tendwa aliyezaliwa mwaka 1950 wilayani Lushoto, Tanga na alifunga ndoa na Aneth Kinabo mwaka 1980, ameacha mke, watoto wanane wa wajukuu 22.