Yannick Bangala avunja mkataba Azam

KIUNGO mkongwe Yannick Bangala amevunja mkataba na klabu ya Azam baada ya kupishana na kocha wake Rached Taoussi.

Bangala ambaye aliichezea Yanga misimu miwili kabla ya kutimkia Azam msimu uliopita tangu atimkie kwa matajiri hao wa Chamazi hajawa na rekodi nzuri kulinganisha na timu aliyotokea.

Katika misimu miwili aliyocheza Yanga alifanikiwa kufunga mabao matatu, huku Azam akifunga moja tu msimu uliopita, huku msimu huu akianza na majeraha.

Ingawa Azam wanafanya siri kubwa, lakini taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata ni kuwa, mkataba wa Bangala na Azam umeshavunjika na kila mmoja kupewa nakala ya makubaliano hayo.

Mmoja wa marafiki wa karibu wa mchezaji huyo ameliambia Mwanaspoti kuwa, sababu kubwa ya Bangala kuchukua maamuzi hayo ni kutokana na kupishana na kocha wa timu hiyo katika moja ya mechi za timu hiyo.

“Kulitokea kupishana kati yake (Bangala) na kocha (Taoussi) sasa Bangala akaona ni bora asitishe mkataba wake na Azam akaongea na meneja wake Faustin (Mukandila) na wakamalizana,” alisema mmoja wa marafiki wa Bangala ndani ya kikosi cha Azam.

“Bado Bangala hajaondoka nchini yupo, tunakutana naye lakini sio ndani ya timu ila baadaye atarudi kwao Kongo kuendelea na mambo mengine.

Azam ilimsajili Bangala akitokea Yanga, ambapo walimsajili kwa kiasi cha sh 20 milioni baada ya kiungo huyo kuingia kwenye utata na uongozi wa klabu hiyo

Tayari Azam nayo imeshafanya maamuzi ya haraka ikimtoa kiungo huyo kwenye usajili wao wa msimu huu na nafasi yake ikachukuliwa na mshambuliaji Alassane Diao.

Diao alishacheza mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Fountain Gate, akifunga bao la pili kwenye ushindi wa timu yake wa mabao 2-0, ambapo kabla hakuwa kwenye usajili wa msimu huu.

Related Posts