Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani humo kufanya doria usiku na mchana katika maeneo yote wanakoishi watu mkoani humo, ili kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wote wa sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.
Pia, amelitaka jeshi hilo kitengo cha usalama barabarani kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto pamoja na kuwasimamia maderava wa vyombo hivyo sambamba na watumiaji wa barabara, ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea katika kipindi hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Desemba 20, 2024, Mtambi amesema uzoefu unaonyesha matukio yanayotishia usalama wa watu na mali zao pamoja na ajali nyingi zimekuwa zikitokea na kusababisha madhara mengi katika kipindi hiki, vitendo ambavyo vinaweza kudhibitiwa endapo mamlaka zinazohusika zitachukua hatua mapema.
“Hakuna sababu kwa wananchi kupoteza maisha au mali zao, kisa eti ni msimu wa sikukuu, msimu huu unatakiwa uwe wa furaha na amani tukiepuka matukio ya aina yoyote yanayoweza kutokea kwa kisingizio cha msimu wa likizo na sikukuu,” amesema Mtambi.
Amefafanua kuwa suala la amani, utulivu na usalama linapaswa kufuata utaratibu na utamaduni wa wakazi wa Mkoa wa Mara katika kipindi chote.
Mkuu huyo wa mkoa, pia amewataka wananchi kutii sheria bila shuruti ili kuepuka usumbufu wowote kutoka kwa vyombo vya dola, ikiwa ni pamoja na kukamatwa na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria huku akipiga marufuku watoto wadogo kwenda kwenye kumbi za starehe.
Amesema wapo baadhi ya watu ambao mara nyingi wamekuwa wakitumia msimu huu kufanya matukio ya uhalifu kama vile wizi, vitendo ambavyo havikubaliki na kuonya kuwa watu wa aina hiyo hawana nafasi ndani ya mkoa huo.
“Kuna wale wanaufanya msimu huu kama wa mavuno, wanavuna kile ambacho hawakukipanda, niwaambie tu kuwa wasithubutu kufanya hivyo kipindi hiki, kwani hatutawaacha salama, Serikali haiko tayari kuona wananchi wanapoteza mali zao au maisha yao kutokana na uwepo wa watu wa aina hii,” amesema.
Mtambi pia amewakumbusha wakazi wa mkoa huo kutunza fedha kwa ajili ya mahitaji ya Januari ikiwepo mahitaji ya shule kwa wanafunzi ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
“Tukumbuke Januari ina mambo yake, kubwa zaidi kuna hili la mahitaji ya watoto wetu kwa ajili ya shule, kwa hiyo tukiwa tunafurahi tukumbuke na kutunza ili mambo mengine yasije yakasimama kwa sababu tumesahau.
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wamesema maagizo hayo yamekuja muda mwafaka na kwamba suala la ulinzi na usalama linapaswa kuwa ajenda ya kudumu na kusimamiwa na kila mmoja katika jamii.
“Utakuta familia nzima inaondoka kwenda kusherehekea sikukuu na kuacha mji wenyewe, mkirudi kila kitu kimeibiwa, sasa hapo wa kulaumiwa ni nani kama sio nyie mlioondoka na kuwatengenezea wezi mazingira ya kuwaibia,” amesema mkazi wa Musoma, Richard Mbusiro.
Mbusiro amesema kabla ya kuacha suala la ulinzi na usalama kwa vyombo vya dola, wananchi wanalo jukumu la msingi kuhakikisha vitendo hivyo havitokei na kwamba wao ndiyo walinzi namba moja wa mali na usalama wao.
Kwa upande wake, Maria Magesa amesema ulevi wa kupindukia ni moja ya changamoto zinazosababisha ajali nyingi nyakati za sikukuu, hivyo ni vema wananchi wakawa makini huku akiomba vyombo vya usalama kuweka ulinzi wa karibu kuepuka watu waliolewa kuendesha vyombo vya moto.