Okoyo azigonganisha timu tatu Ligi Kuu Bara

WAKATI KMC ikiwa kwenye mpango wa kumsajili beki wa kushoto, Deusdedity Okoyo tangu mchezaji huyo aanze kufanya mazoezi na timu hiyo ni takribani siku 10 chini ya kocha Kally Ongala aliyehitaji kumuona kwanza, inaelezwa klabu za Mashujaa na Namungo nazo zinampigia hesabu kumnasa.

Uongozi wa KMC ndio uliomtumia nauli, Okoyo ya kutoka kwao mkoani kwenda jijini Dar es Salaam, makubaliano yaliyotokana na kukaa kwake nje kwa muda mrefu baada ya kumuumia akiwa na JKT Tanzania, hivyo beki huyo alitakiwa afanye mazoezi na timu ili wajiridhishe.

Taarifa za ndani kutoka KMC zilisema walikuwa wakitarajia kukutana naye ili kumalizana naye.

“Leo jioni (jana Alhamisi) tutakutana na mchezaji kufanya mazungumzo ya kumalizana naye, hadi anatumiwa nauli tunaujua uwezo wake, ila tulitaka kujiridhisha na tumeona yupo fiti. Tunahitaji kuimarisha kikosi kupitia usajili wa dirisha dogo, kuna wachezaji wengi tunawaomba kwa mkopo akiwemo kipa wa Simba Hussein Abel, tumepeleka barua ila bado haijajibiwa,” alisema mmoja wa mabosi wa klabu hiyo ya Ligi Kuu Bara, lakini huku kukiwa na taarifa kwamba Mashujaa na Namungo nazo zinamhitaji beki huyo na inaelezwa tayari zimempelekea ofa kwake.

Hivyo, klabu itakayomridhisha kimasilahi, huenda akaanguka saini ili kuanza kuitumikia katika duru la pili la ligi hiyo linalotarajiwa kuanza wiki ijayo.

Related Posts