Same. Ahadi ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kuacha kazi iwapo wananchi wa wilaya za Same, Mwanga na Korogwe hawatapata maji ya uhakika imekufa baada ya huduma kuanza kupatikana.
Kupatikana kwa maji kwa wananchi wa wilaya za Same na Mwanga, mkoani Kilimanjaro na Korogwe iliyoko Mkoa wa Tanga kunatokana na kufikiwa asilimia 99 ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe.
Kusuasua kwa mradi huo, kulisababisha Dk Mpango Machi 21, 2024 aahidi kuacha kazi iwapo haungekwenda vema, akisema hayuko tayari kurudi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kumweleza maji hayatoki.
“Kila mtu atimize wajibu wake, kurudi kwa Rais kwamba maji hayatoki… mimi nitaacha kazi. Hao wengine sijui, katibu mkuu na waziri wake mimi sijui, kwa hiyo tuelewane vizuri,” alisema.
Hatimaye mradi huo uliogharimu Sh300 bilioni sasa umefikia asilimia 99 ya utekelezaji kwa awamu ya kwanza, huku maji yakianza kupatikana kwenye wilaya hizo.
Hayo yamebainishwa jana Desemba 19, 2024 katika ziara ya Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew aliyetembelea mradi huo kukagua maendeleo ya utekelezaji wake.
Mradi huo umeleta manufaa kwa wananchi wa maeneo hayo kwa kuwa wameanza kupata majisafi na salama kwa gharama ya Sh50 kwa ndoo ya lita 20 wakati awali walikuwa wakinunua kwa Sh500.
“Tulikuwa tunapata maji umbali wa kilomita tano lakini kwa kusogezewa huduma hii karibu, sisi kwetu ni sikukuu maana ilikuwa kama huna uwezo wa kufika kilomita tano usingepata huduma ya maji,” amesema Destina Azaliwa mkazi wa Majengo, mkoani Kilimanjaro.
Mkazi mwingine, Ezekiel Michael (70), amesema uhaba wa maji ulikuwa mateso kwake lakini sasa hayapo tena.
Akiwa katika mradi huo, Naibu Waziri Kundo ameziagiza mamlaka zote za maji kuhakikisha zinatoa elimu kwa wananchi wanaokaa karibu na vyanzo vya maji waendelee kuvilinda.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Samemwanga, Rashid Mwinjuma amesema kabla ya mradi huo hali ya upatikanaji maji haikuwa nzuri, lakini sasa mambo ni shwari.
Amesema hali ya upatikanaji wa huduma kwa wilaya za Same na Mwanga kwa sasa ni asilimia 80 kutoka 40 za awali.