Tabora. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameagiza kuondolewa kwa jina la kada wa chama hicho aliyepigiwa kura nyingi za ‘Hapana’ kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, lakini ameteuliwa tena kugombea kwenye uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Kada huyo aligombea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024 katika nafasi ya mwenyekiti wa Kitongoji cha Mkoga kilichopo Wilaya la Mkuranga mkoani Pwani, hata hivyo alipigiwa kura ya Hapana.
Dk Nchimbi amesema jina la mgombea huyo limerudishwa tena kwenye uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika katika kitongoji hicho ndani ya siku 40 baada ya uchaguzi kufanyika, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa.
Amesema hayo leo Desemba 20, 2024 wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho Wilaya ya Nzega mkoani Tabora uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na chama hicho ngazi ya wilaya na mkoa.
Amewataka watendaji na viongozi wa chama hicho nchini kote kujenga utaratibu wa kuteua wagombea wanaokubalika kwa wananchi ili kuepukana na aibu ya wagombea wa chama hicho kupigiwa kura za ‘Hapana’ kwenye uchaguzi.
“Nawataka viongozi wa CCM Mkuranga mkoani Pwani, uchaguzi huo urudiwe na mgombea ambaye alishindwa kwa kura za Hapana asirudie kugombea katika eneo hilo, watafute mgombea anayekubalika na wananchi. Hatuwezi kuendesha chama chetu kwa mazoea na nitafuatilia kuona kama hilo limefanyika,” amesema Dk Nchimbi.
Dk Nchimbi amesema mgombea kukataliwa kwa kupigiwa kura nyingi za Hapana pia ilitokea pia katika Kijiji cha Mgulyati, Wilaya ya Uyui mkoani Tabora ambapo mgombea wa CCM alipigiwa kura nyingi za Hapana na baadae akateuliwa mwingine akashinda uchaguzi, hivyo ni muhimu kuheshimu mawazo ya wananchi.
“Viongozi wa CCM kote nchini mnatakiwa kuteua wagombea wanaokubalika na wananchi ili tusipate idadi ya kura nyingi za Hapana, na tukiteua wale ambao hawakubaliki, tunakuwa hatuheshimu wananchi kwani mwisho wa siku watakataa kupiga kura kwa wagombea wetu,” amesema Dk Nchimbi.
Kiongozi wa dini kutoka Wilaya ya Nzega, Samwel Jukeli amesema kuna haja kwa viongozi kusikiliza matakwa ya wananchi ili kuepuka machafuko ambayo hutokea kwa watu kutoelewana.
“Alichoongea Katibu mkuu wa CCM ni ukweli mtupu kwani hata kwenye vitabu vya dini imeandikwa kwamba matakwa ya wengi ni baraka, hivyo hata vyama vyetu vya siasa vinao wajibu wa kuchagua wagombea wao ambao wananchi wanawataka badala ya kuteua wale ambao hawakubaliki,” amesema.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe, akichangia hoja katika mkutano wa chama hicho, amesema ataendelea kufanya kazi ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zilizopo katika Wizara ya Kilimo anayoisimamia, ili chama hicho kigeuke kero kwa wananchi.
Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amezindua ukumbi wa mikutano wa chama hicho wilayani Nzega, akagawa pikipiki kwa watendaji wa chama hicho zaidi ya 229, pia akakabidhi Sh50 milioni kama mtaji kwa wajasilimali wanawake katika chama hicho, fedha ambazo zimetolewa na Bashe.