Katibu Mkuu wa wizara ya usalama wa ndani Raymond Omollo ametoa onyo kali kwa mashirika yasiyo ya serikali dhidi ya kutumia vibaya fedha za wafadhili kusaidia shughuli haramu, ikiwa ni pamoja na ugaidi.
Amesema baadhi ya mashirika yanatumiwa katika ubadilishaji wa siri wa matumizi ya fedha zinazokusudiwa kwa madhumuni halali. Mashirika hayo yamesajiliwa kwa miradi tofauti lakini yanatumiwa kama njia za kuhamisha fedha haramu kusaidia shughuli za kigaidi.
Amehimiza kukuza uwajibikaji na imani kubwa kati ya mashirika yasiyo ya serikali katika jumuiya ya wafadhili, taasisi za fedha na umma, kwamba fedha zinawafikia walengwa waliokusudiwa.
“Wameshindwa kuwasilisha marejesho yao ya kodi”
Kenya inapoweka jitihada za kushughulikia mapungufu haya, Katibu huyo Mkuu wa usalama anahimiza hitaji la uwazi zaidi. Amesema kuwa serikali imeimarisha ufuatiliaji wa fedha za mashirika yasiyo ya serikali hata kama baadhi yanasalia kusita kufichua vyanzo vyao vya ufadhili.
“Kuna ukosefu wa udhibiti wa kutosha wa ufadhili miongoni mwa baadhi ya mashirika yasio ya serikali yanayofanya kazi, ambao kwa miaka mingi wameshindwa kuwasilisha marejesho yao ya kodi au hata kuwa na ufichuzi wa jinsi wanavyopokea rasilimali zao na jinsi rasilimali hizo zinavyotumika.”, alisema Omollo.
Alikuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya tathmini ya hatari ya ufadhili wa ugaidi.
Haya yanajiri wakati jopo kazi la kimataifa la uangalizi wa fedha kulingana na viwango vya kimataifa dhidi ya utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi Financial Action Task Force (FATF) likiiweka Kenya kwenye orodha ya mataifa yanayofuatiliwa kutokana na mapungufu katika kushughulikia utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi.
Miongoni mwa masuala yaliyoainishwa ni pamoja na, kushindwa kwa Kenya kushtaki kesi za utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi, kutokuwepo kwa kanuni za muongozo wa biashara ya sarafu mtandao yaani (cryptocurrencies) na mashirika yasiyo ya serikali, na uangalizi dhaifu katika sekta ya mali isiyohamishika kama vile ujenzi.
Ripoti ya uchunguzi wa kina
Tathmini hiyo iliongozwa na Kikundi cha Kiufundi kinachojumuisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mashirika ya Manufaa ya Umma (PBORA), iliyokuwa Bodi ya Uratibu ya mashirika yasio ya serikali, Kituo cha Kuripoti Fedha (FRC), Shirika la Kiislamu la Haki za Kibinadamu (MUHURI) na Kituo cha Kitaifa cha Mashirika ya Kiraia cha Kenya (KNCSC).
Walter Mwania, afisa mkuu wa miradi katika shirika lisilo la serikali la Midrift Human Rights Network linalohusika na mapambano dhidi ya ugaidi na itikadi kali anasema ripoti iliyotolewa imefanya uchunguzi wa kina wa mambo yanayofanyika kwenye umma na hivyo wanaiunga mkono.
Pamoja na hayo, Mkuu wa mawaziri nchini Kenya Musalia Mudavadi amesema mashambulizi 47 ya kigaidi katika ardhi ya Kenya yamezuiwa kati ya Januari 2022 na Novemba 2024. Amesema mafanikio haya yaliwezekana kwa ushirikiano na asasi za kimataifa kupitia mafunzo na usaidizi wa vifaa.
“Katika kipindi hicho, magaidi kadhaa wamewaua. Serikali pia imefanikiwa kuhakikisha magaidi 11 wamehukumiwa.”
Musalia ametoa maagizo mapya kwa mamlaka za usalama wakati huu wa msimu wa sherehe ikiwemo kuongeza doria kwenye barabara kuu na kwenye mipaka ya taifa.