Ahadi yatimizwa, wakazi Hanang wakabidhiwa nyumba

Hanang. “Baada ya dhiki faraja.” Methali hii inawiana na hali waliyopitia wakazi wa mji mji mdogo wa Katesh, wilayani Hanang, ambao Desemba 3, 2023 walikumbwa na maafa yaliyotokana na maporomoko ya tope.

Baada ya mwaka mmoja, leo Desemba 20, 2024, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekabidhi nyumba 109 ambapo watu 745 wataishi, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Nyumba hizo zimejengwa kwenye kitongoji cha Waret, katika Kijiji cha Gidagamowd wilayani Hanang, mkoani Manyara.

Pia, amewakabidhi hati za umiliki wa viwanja na majiko ya gesi ya kupikia.

Baadhi ya nyumba zinazokabidhiwa na Serikali kwa waathirika 109 wa tope zilizojengwa kwenye kitongoji cha Waret, Kijiji cha Gidagamowd wilayani Hanang’ mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

Majaliwa alisema fedha za nyumba hizo zimepatikana kutokana na michango iliyotolewa na watu mbalimbali.

“Nyumba hizi ni bora zimejengwa kwa ustadi mkubwa na zinaweza kuhimili matatizo yoyote yakitokea ikiwemo matetemeko ya ardhi,” amesema.

Majaliwa amesema ujenzi wa nyumba 73 kati ya 109 umegharamiwa na Serikali Kuu na kujengwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma-JKT), 35 zimejengwa na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania na moja imejengwa na Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Taifa (UWT).

Amesema Serikali ilitoa Sh1.38 bilioni kwa ajili ya kuweka huduma za kijamii zikiwemo za umeme, maji na barabara.

Waziri mkuu amewaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, kuratibu ugawaji wa viwanja vya ziada vilivyopo eneo hilo ili kuendeleza eneo hilo.

“Tunataka eneo hili lisitambuliwe kama makazi ya waathirika bali kijiji rasmi chenye huduma zote muhimu za kijamii na liwe kielelezo cha maboresho ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote,” amesema.

Amewapongeza walioshiriki uokozi akisema watu 500 waliokolewa baada ya maafa kutokea, tukio lililosababisha

watu 89 kufariki dunia, 139 walijeruhuwa na mashamba ya watu kuharibika, nyumba 261 zilipata madhara ikiwemo nyumba 95 zilizobomoka kabisa.

Amesema miundombinu muhimu ya maji, nishati ya umeme, barabara, zahanati, soko, shule, maeneo ya kuabudu imetengwa kwa ajili ya wakazi wa eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema wananchi wanamshukuru Rais Samia kwa kuwa nao kipindi cha maafa kwa kuahirisha ziara yake ya nje ya nchi na kufika Hanang kuwapa pole.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa kuahidi kuwajengea nyumba na kutekeleza hilo, leo (Desemba 20) umekabidhi hati 109 za nyumba za waathirika wa maporomoko ya tope,” amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi amesema Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu waliwapatia vyakula na magodoro waathirika wa tukio hilo. Alisema jana (Desemba 18) Rais Samia alitoa majiko ya gesi kwa ajili ya wananchi hao.

Katibu Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu, Lucia Sebastian amesema ujenzi wa nyumba 35 uliofanywa na taasisi hiyo unaashiria umoja ambao unawatambulisha kama Watanzania.

“Kwa pamoja tumetoa makazi, tumetoa amani na usalama kwa familia hizi na tumejenga maisha yao upya. Ushiriki wa TRCS katika safari hii umeongozwa na dhamira yetu ya kusaidia jamii wakati wa shida na dharura,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM, John Mongella amesema Katiba ya nchi imeeleza ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma vyema na kwamba, Serikali inayoongozwa na CCM inafanya hivyo.

“Kama chama ujumbe wetu ni kuwa tunaridhishwa na mambo yanayoendelea kwenye Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo kwa kasi zaidi,” amesema Mongella.

Kwa niaba ya wananchi wengine waliokabidhiwa nyumba, Mkazi wa Katesh A, Kizito Mwati ametoa shukrani kwa Serikali kwa kazi kubwa iliyofanya tangu kutokea maafa mpaka sasa wanapokabidhiwa nyumba hizo.

Susan Daqaro, aliyepatiwa nyumba amesema hakutarajia kupata yenye vyumba vitatu, ukumbi, choo na bafu.

Kwa upande wake, Peter Konki ameishukuru Serikali kwa kutimiza ahadi.

Wakati wa maporomoko Desemba 3, 2023 wakazi wa kata tatu za Katesh, Jorodom na Gendabi waliathirika zaidi kutokana na tope zito, mawe na visiki vya miti vilivyoporomoka kutoka mlima Hanang.

Related Posts