Usiyoyajua kuhusu ya msitu wa Galanos Tanga

Tanga. Msitu wa Galanos umebeba siri nyingi. Umekuwa ni msitu wa giza ambao unaficha maovu ya watu na kuibua hofu kwa wananchi wanaouzunga.

Matukio ya mauaji yamekuwa yakifanyika ndani ya msitu huo na wakati mwingine miili ya watu au wanyama waliouawa ikitupwa humo, jambo ambalo limekuwa likiongeza hofu kwa wakazi wa maeneo ya jirani.

Msitu huo unapatikana katika Mtaa wa Nguvumali B ndani ya Halmashauri ya Jiji la Tanga mkoani hapa, ambapo upande mmoja kuna shule ya sekondari ya Galanos, upande mwingine makazi ya watu na sehemu nyingine kwa ajili ya bandari kavu.

Wananchi wanaoishi jirani na msitu huo wamekuwa wakishuhudia matukio mbalimbali ya kutisha yanayofanya wapate hofu, kwani kuna visa vya watu kuuawa na wizi wa mifugo ambayo huchinjwa msituni.

Inaelezwa kuna matukio ya miili ya watu kukutwa ndani ya msitu huo bila kufahamika wameuawa humo au mauaji yamefanyika sehemu nyingine na miili yao kutupwa ndani ya msitu huo huku wahusika wakitokomea.

Wananchi wanasema mifugo inayoibiwa maeneo mbalimbali, masalia yake hukutwa msituni humo zikiwemo ngozi, vichwa na mifupa huku wahusika wakiondoka na nyama ama kwenda kuuza au kutumia wenyewe.

Tukio la mwisho kutokea ndani ya Msitu wa Galanos ni la Septemba 30, 2024 ambapo mwili wa Ali Mohamed maarufu kama Bagidad (60), aliyetuhumiwa kumnyonga mkewe na dada wa kazi, ulikutwa humo ukiwa umeharibika na haikufahamika kama alijiua au aliuawa.

Mkazi wa Nguvumali B, Peter Panga anaeleza kuwa alihamia kwenye eneo hilo tangu mwaka 2014 akifanya kazi ya ulinzi katika moja ya taasisi ya hapo Galanos, na ameshuhudia matukio kadhaa ya uhalifu eneo hilo.

Amesema amewahi kushuhudia matukio matatu ya miili ya watu kutupwa kwenye msitu huo kwa nyakati tofauti, ambapo mwili wa mwalimu mmoja wa Kiyomoni ulikutwa humo, jambo lililoleta taharuki kwa wananchi kwani haikufahamika ulikotoka.

Amesema tukio la pili ni mwanamke mmoja ambaye alikuwa mkulima wa bustani ya mchicha katika eneo hilo, naye aliuawa na watu wasiojulikana na mwili wake kutelekezwa ndani ya msitu huo, kabla ya kubainika siku iliyofuata.

“Matukio mengine ni watu kuvamia usiku na kuiba mifugo yetu, mfano kwangu waliiba nguruwe wangu wawili, nilikuwa lindo nikasikia wanapiga kelele, kufika nakuta damu tu, wamechinja nguruwe wangu na kuondoka na nyama kwenye huu msitu hapa, hivyo mamlaka ziangalie wanatusaidia vipi ili msitu huu usafishwe,” amesema Panga.

Mkazi wa Nguvumali B, Eliaman Majura amekiri kuwepo wa wizi wa mifugo katika eneo hilo, hali ambayo imemfanya aache kufuga kwani ng’ombe wake wote waliibiwa kwa nyakati tofauti, na kuchinjiwa ndani ya msitu huo.

Anasema wamewahi kukuta vichwa na ngozi za ng’ombe ndani ya msitu huo baada ya wamechinjwa usiku.

“Mara nyingine wanachinja ng’ombe ambaye ana mimba, hivyo tunakuta ndama kichakani akiwa ametupwa baada ya kutolewa tumboni kwa mama yake. Nyama inachukuliwa,” amesema Majura akieleza hisia zake kuwa wahusika hawatokei eneo hilo.


Usiyoyajua kuhusu ya msitu wa Galanos Tanga

Akizungumzia matukio hayo, diwani Kata ya Nguvumali jijini Tanga, Selleboss Mustafa amesema ni kweli hayo yanatokea na yeye kama kiongozi wa eneo hilo alishatoa agizo kwa viongozi wote wa mitaa inayozunguka eneo hilo kuziandikia barua taasisi ambazo zina maeneo kwenye msitu huo kuyafanyia usafi.

Amesema anafahamu chanzo cha matukio hayo ni kutokana na msitu huo kuwa mkubwa kiasi kwamba ukiwa huna sababu ya msingi, huwezi kuingia, hivyo mamlaka husika zikisafisha njia na mipaka yake itasaidia kupunguza changamoto hizo.

“Eneo lile kuna mitaa mitatu ambayo ni Nguvumali A, B na Old Nguvumali ambapo sehemu kubwa ya maeneo haya kwa sababu ya maporomoko yanalindwa na miti, na ni kweli ni sehemu hatarishi kwa kutokea matukio ya mauaji,” amesema Mustafa.

Mkuu wa wilaya ya Tanga, Jaffar Kubecha alipoulizwa, awali hakutaka kuzungumzia msitu huo hadi atakapoutembelea, hivyo, Desemba 16, 2024, alimchukua mwandishi wa Mwananchi na wajumbe wa kamati ya usalama kwenda kuutembelea.

Baada ya kuutembelea, Kubecha na kamati yake walibaini ukweli wa kuwepo matukio hayo ya uhalifu ikiwemo kutupwa miili ya watu, wizi wa mifugo na mazingira ambayo yanahitaji kufyekwa na kuwekewa taa ili kuwa salama wakati wote.

Kubecha amewatoa hofu wananchi kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vipo kazini na vitashughulikia changamoto zote zilizotajwa ili kuona namna zitakavyotatuliwa kupitia taasisi zilizopo humo.

Ameziagiza taasisi zenye maeneo ndani ya msitu wa Galanos kusafisha mipaka na maeneo yote yanayozihusu ili kuwa safi na salama kwa watu wanaopita na kuishi hapo, kwa lengo la kuhakikisha usalama wao.

Amemtaka Mkurugenzi wa jiji kutoa agizo kwa wananchi wote wenye viwanja ndani ya mitaa inayopakana na msitu kuwa wapewe notisi ya kuvifanyia usafi, na atakayeshindwa hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao, ikiwemo kunyang’anywa viwanja.

Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Tanga, Inspekta Victor Lupondo ameongeza kuwa ili kuhakikisha usalama wa eneo hilo, watakuwa wakifanya doria ya mara kwa mara kama awali kwani walikuwa wakifanya hivyo.

Amewahakikishia wananchi doria hiyo itaweza kuthibiti matukio ya uhalifu yanayotajwa kufanyika humo, hivyo ameshauri wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida kwa kuwa hatua zitaanza kuchukuliwa mara moja.

Kaimu Mkurugenzi Jiji la Tanga Ali Mweta amesema wanaandaa utaratibu wa kuwapa taarifa wote wenye maeneo mitaa inayozunguka msitu wa Galanos, waendeleze viwanja vyao kama sheria inavyowataka.

Related Posts