Vigogo wa dawa za kulevya kubanwa kila kona

Dar es Salaam. Ni kibano kila mahali. Ndiyo inaweza kuwa tafsiri ya kilichofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) baada ya kuingia makubaliano na Shirika la Posta Tanzania (TPC) kudhibiti usafirishaji wa dawa hizo kupitia vifurushi.

Hatua hiyo imefikiwa kufuatia kuwepo kwa wimbi la watu wanaosafirisha dawa za kulevya kupitia vifurushi na mizigo kupitia posta.

Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi za DCEA imebainika kuwa wahalifu wamekuwa wakitumia mbinu za kusafirisha dawa za kulevya kupitia vifurushi na mizigo.

Katika kipindi cha mwaka mmoja 2024 dawa zilizokamatwa ni mirungi (kilo 39,928.99), heroini (gramu 1,304.17), kokaine (gramu 673.55) na dawa tiba zenye asili ya kulevya kama morphine na codeine.

Kufuatia hilo, leo Desemba 20, DCEA imesaini hati ya makubaliano na TPC ikilenga kuimarisha udhibiti wa usafirishaji wa dawa za kulevya, kemikali bashirifu, na dawa tiba zenye asili ya kulevya kupitia mtandao wa posta.

Postamasta Mkuu, Macrice Mbodo amesema Shirika la Posta limejipanga kuhakikisha usalama wa usafirishaji wa bidhaa kupitia mtandao wake.

Akirejea sheria na miongozo ya kitaifa na kimataifa, amesema mtandao wa Posta hautaruhusu bidhaa haramu kama dawa za kulevya, silaha na nyara za Serikali kupita bila kugundulika.

“Teknolojia ya kisasa imerahisisha usafirishaji wa dawa mpya za kulevya kupitia mifumo ya kifedha ya kidijitali na majukwaa ya siri,” amesema Mbondo.

Hata hivyo, Mbondo amesema mtambo wa kisasa uliotolewa na DCEA umeimarisha uwezo wa TPC kubaini dawa hizo bila kufungua vifurushi, hatua ambayo ambayo ameitaja kama nyenzo muhimu ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema ushirikiano huo utahusisha mafunzo ya watumishi, kuboresha vifaa vya utambuzi, na kubadilishana taarifa kwa wakati ili kuimarisha ufanisi wa ukaguzi.

Amesema ushirikiano huo ni kengele ya tahadhari kwa wahalifu na unatoa ujumbe kwa waliokuwa wakitumia mbinu hiyo kusafirisha dawa za kulevya.

“Niendelee kutoa shukrani kwa wadau wote wanaoshiriki katika vita dhidi ya dawa za kulevya, akiwataka Watanzania kutoa taarifa za wahalifu na kushirikiana na Serikali kuhakikisha mtandao wa posta unabaki salama,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Related Posts