Arusha. Wakati kesho Desemba 21, 2024 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akitarajiwa kutegua kitendawili cha kutetea nafasi hiyo au la, viongozi waandamizi wa zamani wa chama wanashauri ajiweke kando.
Wanashauri Mbowe kutumia busara kwa kusikiliza ushauri wa familia yake, iliyomtaka apumzike uongozi.
“Nimekuwa na wakati mgumu na familia yangu. Hakuna kipindi familia yangu imenikalia mguu pande kama kipindi hiki, wananiambia; baba inatosha, toka achana na siasa rudi nyumbani uendelee na maisha mengine.
“Sasa familia yangu nayo ina nguvu katika maisha yangu, lakini vilevile na familia ya Chadema nayo ina nguvu sasa,” alisema Mbowe Desemba 18, 2024.
Kauli hiyo aliitoa alipozungumza na wenyeviti wa mikoa na wanachama waliofika nyumbani kwake Mikocheni, Dar es Salaam kumshawishi achukue fomu kutetea nafasi hiyo, wakisema bado wana imani naye na hawajamuona mwingine anayeweza kuvaa viatu vyake.
Kesho (Jumamosi Desemba 21), saa 48 alizotoa Mbowe akiwaomba viongozi hao kumpa muda wa kutafakari ombi lao unakwisha na anatarajiwa kutoa msimamo wa kugombea au kutogombea atakapozungumza na wahariri na waandishi wa habari nyumbani kwa Mikocheni.
“Ninachowaahidi kuwa sitaingia kwenye vita ya kukipasua chama, nitaingia kwenye vita ya kukijenga chama chetu. Kuanzia sasa (Jumatano) hadi Jumamosi nitakuwa nafuatilia kwa karibu mambo yanavyokwenda, nikiona chama kinakwenda shimoni, Kamanda nitaingia mzigoni,” alisema Mbowe.
Mbowe aliyechaguliwa uenyekiti kwa mara ya kwanza mwaka 2004, atavunja ukimya wa uamuzi wake iwapo atatetea nafasi hiyo ili kuongoza Chadema kwa miaka mitano ijayo.
Wakati Mbowe akisubiriwa kutoa uamuzi, aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Profesa Abdallah Saffari akizungumza na Mwananchi amesema tatizo siyo Mbowe bali watu wanaomzunguka aliowaita ‘machawa’.
Amemuomba Mungu kumpa hekima mwenyekiti huyo, kati ya leo na kesho ili kutoa uamuzi sahihi.
“Asikilize familia yake, kama alivyotamka siku ile mbele ya vyombo vya habari. Kama ni kweli familia yake ilisema hivyo, basi aisikilize… ndio watu muhimu kuliko wengine. Ningekuwa mimi ningeisikiliza familia yangu ilivyonishauri kutogombea,” amesema.
Amesema anayeweza kutengeneza au kuivunja Chadema ni Mbowe na kwamba uamuzi upo po mikononi mwake.
Kwa mujibu wa Profesa Saffari, Mbowe akiamua kuendelea na uongozi, basi chama hicho kikuu cha upinzani nchini hakitakuwa na tofauti na vyama vingine vilivyovuma lakini hivi sasa vimefifia.
Profesa Saffari amesema endapo Tundu Lissu akishinda uongozi utakuwa wa tofauti, hivyo watu wanaomzunguka Mbowe hawawezi kukubali makamu huyo ashinde uenyekiti.
Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), ameshachukua na kurejesha fomu kuwania uenyekiti wa chama hicho taifa.
“Siyo mimi ninayesema hivi, bali wapo watu wengi wenye heshima zao siwezi kuwataja wanaongea hili, ingawa inahitaji akili nyingine na weledi kuona kitu kama hicho,” amesema.
Profesa Saffari ambaye ni mtalaamu wa sheria na diplomasia, amesema amesikiliza hotuba ya Lissu akisema kunapokuwa na kitu kigumu unapaswa kuandika, kisha unasoma mbele ya umma badala ya kuzungumza tu.
“Ukiwa huru kuzungumza pasipo kuwa na hotuba kuna kuteleza ulimi na kusababisha matatizo makubwa,” amesema.
Katibu mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa amedai kutokana na kinachoendelea ndani ya Chadema, alishamuandikia ujumbe mfupi (sms) Mbowe akimshauri haoni tija kiongozi huyo kuwania uenyekiti kwa miaka mingine mitano.
“Nimemtumia ujumbe bila kumungu’nya maneno wala kuficha pembeni kwamba kwa uhai wa chama hata kama siyo Chadema, lakini ni mpenzi wa Tanzania inayohitaji kukombolewa kutoka mikononi mwa CCM,” amedai.
Dk Slaa amesema: “Nimemwambia siyo tija kwa yeye kugombea baada ya miaka 20, kutakuwa hakuna tofauti kunga’nga’nia nafasi au Mbowe atueleza anataka nini. Nimemuuliza unagombea kwa manufaa ya nani ya kwake au Tanzania?”
Slaa aliyewahi kuwa mbunge Karatu amesema kama anagombea kwa manufaa ya Tanzania, basi ni vyema akajitafakari kwa sababu alipoingia kwenye maridhiano inadaiwa amesababisha madhara kwa Chadema.
“Mbowe ni mzoefu ndani ya Chadema ajaribu kuhesabu kura za mkutano mkuu anaweza kupata kura ngapi. Nimemtumia jana (Desemba 18) ujumbe,” amesema.
Hata hivyo, Dk Slaa amesema wapigakura wataamua kwa sababu siyo wajinga kwamba, wale wa 2014 wapo tofauti na mwaka 2024.
Mchambuzi wa siasa, Deus Kibamba amesema kwa asilimia kubwa, katiba za vyama vya siasa hasa vya upinzani hazipo vizuri, akitoa mfano kunapotokea sintofahamu hakuna vyombo vinavyoweza kurudisha hali ya kawaida.
“Utakuta vyombo vimetajwa katika katiba za vyama, lakini havina uwezo. Chombo kinalishwa na mwenyekiti au makamu mwenyekiti. Tatizo lipo kwa Afrika watu wana nguvu kuliko taasisi husika.
“Ushauri wangu kwa Chadema, huu muda umewafundisha, wanatakiwa kuunda jopo la wazee wa chama litakalowaita hawa wanaonyukana (Lissu na Mbowe) na kuwasikiliza ili Chadema kipite salama wakati huu, hata baada ya wakati huu.
“Katika nchi nyingine chombo au baraza la kushauri chama na kuwavusha kwenye hali ngumu siyo lazima liwe na wanachama peke yake, bali linaweza kuwa na watu mashuhuri na huru wanaotoka kwenye vyama vingine au kutokuwa na chama,” amesema.
Kwa mujibu wa Kibamba, kwa namna Chadema watakavyoutatua mgogoro huo, utaanzisha mfano mzuri kwa vyama vingine vitakavyoweza kutatua changamoto zitakazowakabili kwa nyakati tofauti.