Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imejiwekea lengo la kukusanya Sh15.27 trilioni katika kipindi cha miezi sita kuanzia Januari hadi Juni 2025.
Mbali na hilo mamlaka hiyo imejiwekea lengo la kukusanya Sh3.46 trilioni katika mwezi wa Desemba kiwango ambacho hakijawahi kukusanywa tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Fedha wa TRA, Dinah Edward alipoongoza timu ya viongozi wa mamlaka hiyo iliyokwenda kutoa shukrani kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ushirikiano iliyowapa mwaka 2024.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa ushirikiano huo umechangia kwa kiasi kubwa kuiwezesha TRA kuvuka lengo la makusanyo ya kodi kupitia jukumu hilo walilokasimiwa kisheria.
Amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025 mamlaka hiyo ilikuwa na lengo la kukusanya Sh31.05 trilioni na katika kipindi cha miezi mitano kufikia Novemba imekusanya Sh12.64 trilioni sawa na asilimia 41.67 ya lengo kuu.
“Ufikiwaji wa lengo hili kufikia Juni 2025 inahitaji ushirikiano na walipa kodi na wadau mbalimbali wanaohusika katika mnyororo mzima wa ukusanyaji wa mapato.
“Ushiriki wa BoT umejipambanua katika maeneo ya kisera, utendaji na usimamizi wa benki, uhamalishaji wa fedha na maeneo mengine mengi. Yote haya yana mchango chanya katika kupanua wigo wa kodi, kuleta wepesi kwenye ulipaji wa kodi na kuboresha usimamizi wa mapato,”
Kwa upande wake Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema benki hiyo itaendelea kutekeleza wajibu wake kuhakikisha hakuna changamoto katika mifumo ya malipo ili kuwezesha TRA kukusanya kodi kwa mujibu wa sheria.
Tutuba amesema BoT kama taasisi inayohusika na usimamizi wa sekta ya kifedha imeendelea kujihimarisha kuhakikisha sekta hiyo inakuwa imara kuwezesha shughuli za kiuchumi kutekelezeka.
“Sisi tumejipanga vizuri mifumo yetu iko imara na madhubuti kuhakikisha mtu anapotaka kulipa kodi kwa njia yoyote anafanya malipo na yanaingia kwenye akaunti za Serikali,” amesema.
Amesema benki hiyo inahakikisha usalama wa akaunti zote zikiwamo za Serikali na benki hizi zote.
“Idara yetu inayohusika na ufuatiliaji wa mifumo ya mtandao inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha hakuna anayeweza kuiingilia. Tumesikia changamoto katika baadhi ya nchi lakini niwahakikishie Watanzania mifumo yetu BoT iko salama na tunaendelea kuifuatilia wakati wote,” amesema Tutuba.
Gavana huyo pia ameipongeza TRA kwa kubadili mfumo wa ukusanyaji kodi ikiwemo kupunguza matumizi ya nguvu na mabavu hali inayofanya watu kuanza kuwa na utaratibu wa kulipa kodi kwa hiari.
“Tunapata taarifa kwamba licha ya kuwa bado ni watoza ushuru lakini marafiki, sasa huu urafiki unawafanya watu waone wajibu wao kulipa kodi na hata wale wenye changamoto waone kuna nafasi ya kukaa chini na kuzungumza,” amesema Tutuba.