MCT yaja na mfumo mpya tuzo za Ejat, wadau waujadili

Dar es Salaam. Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeahirisha ufunguzi wa dirisha la Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (Ejat) mpaka Aprili, 2025.

Dirisha hilo ambalo hufunguliwa kati ya Novemba na Desemba kila mwaka, limeahirishwa, ili kufanya utafiti wa namna bora za kupata washindi wa tuzo hizo, tofauti na mfumo ulizoeleka.

MCT imekuwa ikitoa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari kwa miaka 15 tangu 2009 kwa kukusanya habari zilizochapishwa kutoka kwa waandishi wa habari wa magazeti, radio, televisheni na mitandaoni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 20, 2024 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura amesema watafanya utafiti wa kuwatambua waandishi zaidi wa habari, hata wale wasiowasilisha kazi zao.

“Utafiti wa tuzo hizi utafanyika kitaifa kuanzia Januari hadi Machi, 2025 na utaenda sambamba na mpango wa mabadiliko ya kimfumo, ili Baraza lifanye kazi kidigitali na kwa ukaribu na wananchi,” ameeleza.

Amesema moja ya mambo yatakayofanyiwa utafiti ni pamoja na muundo wa tuzo, namna ya kupata washindi na ushirikishwaji wa wananchi katika habari zenye suluhisho kwa changamoto za kijamii.

“Baada ya mfumo huu wa utoaji tuzo kutumika kwa miaka 15, Baraza litafanya marekebisho ili kumfikia kila aliyeshiriki kukamilisha habari hiyo,” ameeleza.

Sungura ameongeza kuwa moja ya namna itakayotumika kupata washindi, ni kufuatilia na kujua habari bora za mwandishi, pasipo wao kujua, tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo wanahabari hupeleka kazi zao wenyewe.

“Kuna waandishi wengi wenye kazi nzuri ambao hawajawahi kuwasilisha kazi zao kwa Baraza ili kupata tuzo, lengo letu ni kuibua kila mwandishi mwenye kazi nzuri,” ameeleza.

Pia ameeleza kuwa kuna baadhi ya makundi yaliyosahaulika, ambao nao wanahusika katika habari zilizoshinda.

“Tuzo zinawahusu wapiga picha, wasoma habari, watangazaji wa habari za michezo,” anasema.

Kadhalila Sungura amesema, baada ya utafiti huo mwaka 2025, tuzo hizo zitatolewa kwa habari nzuri za mwaka 2024 na 2025.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Sungura amesema washindi wa jumla kwenye tuzo mbalimbali watagombea tuzo za kimataifa.

“Mshindi wa jumla kazi zake zitapelekwa kwenye tuzo za Afrika Mashariki,” ameeleza.

Akizungumzia utaratibu huo wa MCT, mwanahabari na mshindi wa tuzo za EJAT mwaka 2011, Neville Meena ameukosoa akisema si vyema kutumia kura katika kupata washindi wa tuzo hizo.

“Mfumo wa mwanzo ulikuwa na vigezo na masharti ili kushinda, sidhani kama kushirikisha wananchi katika kufanya maamuzi kutaleta washindi stahiki wa tuzo hizo,” amesema.

Anasema mfumo wa kura wengi huzipiga kwa mapenzi na si vigezo vya kitaaluma.

 “Kwangu mimi mfumo wa mwanzo ni mzuri zaidi na ulileta washindi wanaostahili tuzo hizo,” ameeleza.

Meena ameongeza kuwa, suala la tuzo linapaswa lifanywe kwa utulivu na lifanywe na wanaojua taaluma hiyo na si mapenzi kwa waandishi.

Pia, amesema Tanzania ina vyanzo vingi vya habari na hadhani kama vitafuatiliwa kwa weledi ili kupata mshindi.

“Kuna blog, magazeti, televisheni, instagram na vingine vingi na kuna habari za kila aina, si rahisi kufuatilia habari zote na kupata mshindi, naona ni bora mfumo wa zamani ukatumika,” ameeleza.

Si vibaya kuboresha mfumo

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation, Dastan Kamanzi amesema uamuzi wa baraza hilo ni mzuri katika kuboresha tuzo hizo.

“Ni kwa muda mrefu tuzo za Ejat zimefanyika kwa mfumo uleule na kujenga mazoea kwa waandishi kama Baraza ilibidi wajitathimini ili kuleta utofauti na wamefanya hivyo,” ameeleza.

Amesema, hata hivyo kulikuwa na maswali ya wadau mbalimbali wa habari kuhoji mchakato wa wanahabari kushinda tuzo hizo.

“Si tu wadau, hata majaji pia wanakiri kuwa habari nyingi hazijakidhi vigezo vya kushinda tuzo, mara nyingi wanawapa ushindi wale wenye uafadhali tu,” ameeleza Kamanzi.

Kamanzi amesema, kushirikisha umma katika kufanya maamuzi ni jambo sahihi zaidi na kuwa habari hizo zinaandikwa kutatua changamoto zao.

“Mfumo huu utahamasisha waandishi kufanya kazi zenye ubora na zenye faida kwa umma,” ameeleza Kamanzi.

Related Posts