Dodoma. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ilingo, Kijiji cha Msagali wilayani Mpwapwa, Alex Chikumbi amesimulia ilivyokuwa wakati wa tukio la mauaji ya askari polisi wawili na mtuhumiwa wa unyang’anyi, Atanasio Malenda.
Tukio hilo lilitokea Desemba 18, 2024, wakati Koplo Jairo Kalanda na Konstebo Alfred John walipokwenda kumkamata mtuhumiwa huyo.
Chikumbi amesema askari walikuwa wamejipanga kumkamata Malenda lakini walipofika eneo la tukio, mtuhumiwa alijaribu kupambana nao.
Katika harakati hizo, polisi hao wawili walipoteza maisha pamoja na mtuhumiwa mwenyewe.
“Hili lilikuwa tukio la kushtua kijiji chetu. Tulishuhudia jinsi hali ilivyokuwa mbaya na hatutarajii mambo kama haya kutokea tena,” amesema Chikumbi.
Tukio hili limeacha simanzi kubwa kwa familia za polisi waliopoteza maisha, huku mamlaka zikiendelea na uchunguzi wa kina kubaini chanzo halisi cha mauaji hayo.
Katika tukio hilo, Koplo Msuka na mgambo wa kijiji hicho, Masima Nyau walijeruhiwa na walipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa.
Juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi alisema askari hao waliuawa walipokuwa kwenye mapambano ya risasi na mtuhumiwa aliyedaiwa kujeruhi na kupora Sh2 milioni.
Kamanda Katabazi alisema Malenda alifariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa mapambano hayo.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dodoma leo Desemba 20, Chikumbi amesema saa 1:00 jioni Desemba 17 alipigiwa simu na askari wa upelelezi akimweleza kuna mtuhumiwa aliye kitongojini kwake.
Amesema baada ya ujumbe huo, aliwaeleza mbona hamfahamu mtuhumiwa huyo, lakini walimweleza asubiri hadi watakapofika watamueleza.
“Nikawahoji je, mtendaji anazo taarifa? wakasema wanampigia simu lakini hapokei. Nilikaa hadi nikasinzia. Waliponipigia nikawauliza tena kama wameshampata mtendaji, walinijibu hapokei,” amesema.
“Niliwaambia mtakapokuja mimi mtuhumiwa simjui lakini wao wakasema tutakupa maelekezo kwa upande wa mwenyekiti mwenzako. Nikasema sawa, wakampigia (mwenyekiti wa kitongoji kingine) akasema sawa akawaelekeza (askari)” amemsema.
Chikumbi amesema mbali ya maelekezo hayo, mwenyekiti huyo aliwapa kijana ambaye alifika katika kitongoji hicho saa 3:00 usiku akilenga kuwaelekeza polisi nyumbani kwa mtuhumiwa huyo.
Amesema alimpigia askari jamii (mgambo) Nyau aliyefika nyumbani kwake na kumwelezea kuhusu tukio hilo, iliwalazimu waambatane na askari kwenda kumkata mtuhumiwa.
“Alikwenda kuvaa jaketi na kurudi. Ilipotimia saa 7:00 usiku askari walipiga simu na kumwambia wameshafika kilomita 387, nikawaambia wameshapita wameingia eneo jingine. Niliwaelekeza wakarudi hadi eneo lililoangukia treni,” amesema.
Chikumbi amesema walifika askari watano na kijana aliyekuwa akiwaonyesha kwa mtuhumiwa aliwaambia ana nyumba mbili (wake wawili), hali iliyowafanya kujigawa katika makundi mawili.
Amesema yeye na askari jamii (mgambo) waliondoka na askari wawili na kijana aliyekuwa akionyesha nyumba alibaki na askari watatu.
Amesema kijana na askari watatu walipokwenda kugonga, mkewe alijibu hayupo katika nyumba hiyo bali yuko katika nyingine.
“Walipojibiwa yupo nyumba kubwa, walikuja kuungana nao na kushirikiana kugonga geti. Bwana fungua, mimi mwenyekiti toka nje, tukagonga kimya, maaskari wakazunguka nyuma wakaanza kugonga kwenye madirisha,” anasimulia.
Amesema baada ya kugonga kwa muda wa takribani saa moja bila majibu wakaamua kubomoa geti na kuingia askari wawili na wengine walizunguka nyuma ya nyumba wakihofia mtuhumiwa anaweza kutoka kupitia dirishani.
“Wakakuta geti la pili wakaanza kugonga fungua, kimya wakalifumua. Baada ya kulifumua geti hilo kumbe jamaa alikuwa amejiandaa yuko getini akiwa amebeba panga. Lilipofunguka tu wakaanza kupambana,” amesema.
Ameeleza askari aliyekuwa na bunduki alishika silaha hiyo kwa mkono mmoja, huku akijikinga mapanga ili amshike lakini bahati mbaya alikatwa mkono uliokuwa na bunduki, hivyo ilimlazimu kuiachia.
“Baada ya kuiachia bunduki, kijana huyo aliiokota akawa pia na panga. Silaha zote akawa nazo ikabidi tuanze kukimbia. Kufika katika mlango watu wanapita kama watano lakini kwa bahati mbaya askari jamii aliwahiwa akapigwa panga mguuni,” anaeleza.
Anasema askari jamii akawa anajikinga na mikono ili asikatwe kwa panga kwenye shingo, matokeo yake alikatwa mikononi na jingine likafika pembeni ya shingo.
“Akaona anachelewa, wale askari wako nje aliokota bunduki akaanza kuwakimbiza ndipo kelele ikaanza, akafyatua risasi. Askari wawili waliuawa kwa risasi palepale, mmoja ndiyo tulimbeba majeruhi hadi Hospitali ya Mpwapwa,” anasimulia.
Anasema kwa mujibu wa kijana aliyefika kuwaonyeshea polisi mtuhumiwa huyo alifanya tukio la kupiga kijana mwenzao na kumpora fedha.
“Alisema alikuwa na mzigo wake njiani wakampora na mtuhumiwa alikuwa na vijana wengine kama watano wakati wanampora fedha hizo. Ndiyo maana alikuwa anajua, walikuwa wanamwinda mchana hakamatiki ndipo walipokuja usiku,” anasema.
Anaeleza baada ya tukio hilo ilichukua muda hadi kusogea eneo la tukio kwa kuwa walikuwa wanadhani bado bunduki ina risasi.
Amesema walipoona ameshaondoka katika eneo la tukio, walisogea kuwabeba majeruhi ili kuwaweka ndani ya gari.
“Yule mhalifu alikimbia na pikipiki. Kituoni polisi mtuhumiwa alikuwa na wenzake watano. Alienda kuripoti kuwa wamevamiwa na majambazi baada ya kuelezea kitongoji gani wakaelezwa huko maaskari wamekwenda kuna kazi na mliua askari. Subirini hapo wanakuja wako hospitali,” amesema.
Amesimulia muda mfupi yeye akiwa na askari wengine walifika kituoni hapo na kukutana na mtuhumiwa akiwa kwenye bodaboda akieleza ameumia kwenye tukio.
Amesema hakujua mtuhumiwa alipelekwa wapi baada ya wao kurudi katika eneo la tukio kufuata bunduki iliyoachwa na mtuhumiwa huyo.
Alipoulizwa mtuhumiwa alikuwa akijishughulisha na nini, Chikumbi amesema alikuwa mkulima na mfanyabiashara wa duka lililokuwa katika kijiji hicho.
Hata hivyo, amesema hajawahi kusikia habari za kijana huyo kuhusika na uhalifu wala kushtakiwa katika serikali ya kitongoji.
Chikumbi amesema mgambo aliumia mikono yote miwili na mguu mmoja wa kushoto.
“Hospitali ya Mpwapwa waliamua kumfunga kwenye mguu hadi kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako alifanyiwa kipimo cha X-Ray na baadaye alikatwa mguu.
Amesema alifanyiwa upasuaji usiku wa juzi kuamkia jana (Desemba 19) na kumkata mguu. Mikono ilishonwa majeraha.
Chikumbi amesema hadi kufikia jana (Desemba 19) alikuwa ametumia Sh305,000 kwa ajili ya matibabu.
“Hadi hivi sasa sina fedha za kumsaidia kwenye matibabu. Naiomba Serikali na watu wenye mapenzi mema wamsaidie huyu askari jamii aweze kutibiwa,” amesema.
Koplo Kalanda alisafirishwa kwenda mkoani Rukwa kwa maziko, huku Konstebo John akisafirishwa kwenda Sirari wilayani Tarime mkoani Mara kwa mazishi.
Kabla ya kusafirishwa miili iliagwa jana (Desemba 19) wilayani Mpwapwa ambako Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu wa Jeshi la Polisi, Tatu Jumbe alilaani tukio hilo na kuhimiza jamii kufichua tabia zisizo za kawaida miongoni mwao.
“Nawasisitiza askari wetu kuendelea kuwa waangalifu na kutumia weledi wenu mnapokuwa kazini. IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi) amenituma niwaambie msikate tamaa na endeleeni kutimiza wajibu wenu kwa haki,” amesema.