Wajerumani wakasirishwa na Musk kuinga mkono AfD – DW – 20.12.2024

Katika ujumbe wake ulioandikwa kwenye sentensi moja fupi, Elon Musk amesema, ”Ni AfD pekee inayoweza kuiokoa Ujerumani”.

Hii si mara ya kwanza kwa tajiri huyo namba moja duniani kuunga mkono vyama vyenye sera za kupinga wahamiaji barani Ulaya.

Mwezi uliopita alipigia kampeni kufukuzwa kwa jaji wa Italia, aliyetilia shaka sera ya serikali ya nchi hiyo dhidi ya uhamiaji wa kiholela.

Soma pia: Scholz akiri matokeo yaliyokipa ushindi chama cha AfD yanatia wasiwasi

Wanasiasa wa Ujerumani wamemkosoa Elon Musk, wakisema alichokifanya ni uingiliaji wa siasa za ndani za nchi yao, ambayo inaandaa uchaguzi wa bunge mapema mwakani.

Kombo Picha I Wagombea Ukansela wa Ujerumani 2024
Picha muunganiko ya wagombea ukansela wa Ujerumani – Olaf Scholz (juu kushoto) wa chama cha SPD, Friedrich Merz (juu kulia) wa CDU, Robert Habeck (chini kushoto) na Alice Weidel (chini kulia) wa AfD.Picha: photothek/dpa/picture alliance

Maoni ya Wabunge Kuhusu Kauli ya Elon Musk

Clara Bünger wa chama cha mrengo wa kushoto alieleza kuwa kauli hiyo ni uingiliaji wa wazi, lakini haina uzito wowote kwani Musk hana uelewa wa mfumo wa siasa za Ujerumani.

Alexander Throm wa chama cha kihafidhina CDU, alisema ameshangazwa na kauli hiyo, akisisitiza kuwa mabadiliko yanaweza kufanywa tu na chama kilicho madarakani, na kusisitiza kuwa chama cha AfD hakitaingia serikalini kwa sababu hakuna chama kingine tayari kushirikiana nao.

Soma pia: Chama cha Mbadala kwa Ujerumani AfD chashinda uchaguzi Thuringia

Anton Hofreiter wa chama cha walinzi wa mazingira alikemea vikali, akiwataja mafashisti kama wasaliti wanaoungwa mkono na mabilionea wa mrengo wa kulia kama Musk, akiashiria pia msaada wao wa awali kutoka kwa Putin.

Kauli hizi zinaonyesha mitazamo tofauti ya wanasiasa juu ya ushawishi wa bilionea huyo katika siasa za Ujerumani.

Ujerumani | Mkutano wa chama cha AfD mjini Erfurt.
Chama cha AfD kinadai kutanguliza maslahi ya Ujerumani, lakini sera yake kuu ni kupinga uhamiaji na kuchukia Uislamu.Picha: Sean Gallup/Getty Images

Scholz: Hata mabilionea wana uhuru wa maoni

Hata Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameelezea mtazamo wake kuhusiana na ujumbe huo wa Musk.

Scholz amesema uhuru wa watu kutoa mawazo unawaruhusu pia mabilionea kusema fikra zao, hata ikiwa fikra hizo sio sahihi na hazina maudhui yoyote yenye tija kisiasa.

Chama cha AfD alichokimwagia sifa Elon Musk kinaendesha siasa zake kwa misingi ya chuki dhidi ya wahamiaji, na pia kinapinga Umoja wa Ulaya.

Soma pia: Wajerumani weusi wahofia ushindi wa AFD majimbo ya mashariki

Katika kura za maoni kipo katika katika nafasi ya pili, huku Ujerumani ikielekea katika uchaguzi wa Februari 23 mwakani, ulioitishwa mapema baada ya kusambaratika kwa serikali ya muungano wa vyama vitatu iliyoongozwa na Kansela Olaf Scholz.

Uungwaji mkono wa AfD mashariki mwa Ujerumani

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Bilionea Elon Musk ambaye ni mpambe wa rais mteule wa Marekani Donald Trump, tayari amekwishaviunga mkono vyama vingine vya mrengo mkali wa kulia katika mataifa tofauti barani Ulaya.

Related Posts