Simba yafuata fundi Uganda | Mwanaspoti

KIKOSI cha Simba kipo mjini Bukoba, mkoani Kagera kumalizana na wenyeji wao, Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini unaambiwa mabosi wa klabu hiyo wanapiga hesabu kali ya kuimarisha kikosi hicho kama mapendekezo ya kocha Fadlu David na sasa imevuka mpaka hadi Uganda kufuata fundi wa mpira.

Ndio, baaada ya kumnasa Ellie Mpanzu ambaye inaelezwa huenda leo Jumamosi akavaa uzi mwekundu na mweupe pale Kaitaba kwa mara ya kwanza katika mechi za Ligi Kuu, lakini inampigia hesabu ya kumshusha kiungo mshambuliaji, Allan Okello anayetumia pia mguu wa kushoto kama Mpanzu, ili kuja kuongeza nguvu.

Okello, mwenye umri wa miaka 24 amewahi kupita KCCA na Paradou zote za Uganda kwa sasa anakipiga Vipers iliyopo Ligi Kuu ya nchi hiyo, anayetajwa ni fundi wa mpira kwelikweli kwani analijua boli na inaelezwa kama atashuka Msimbazi na kuungana na wachezaji waliopo basi balaa litakuwa kubwa kwa wapinzani siku watakapokutana uwanjani iwe katika Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho nchini au lile ya CAF, ikiwa Kundi A.

Inaelezwa, Wekundu hao wanamtaka Okello kama kiungo mshambuliaji  ili kuja kukiboresha kikosi chao kupitia dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Desemba 15.

Hatua nzuri kwa Simba ni kwamba kama itampata fundi huyo atatumika moja kwa moja katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kwani Vipers haikushiriki mashindano hayo msimu huu.

Utata pekee wa Simba kumpata Okello ni uwepo wa Rais wa klabu hiyo, Lawrence Mulindwa ambaye amekuwa mtata kuachia mastaa wake muhimu wa kikosi hicho kuuzwa.

Mulindwa ndiye aliyeweka ngumu kumuachia aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo Cesar Manzoki aliyekuwa anawindwa na Simba akitaka fedha ndefu kisha baadaye kumuuza China.

Simba ilifanya juhudi kubwa kumnasa Manzoki ambaye naye alishakubali karibu kila kitu kujiunga na wekundu hao ikiwamo kuja mpaka Tanzania lakini bosi huyo akaweka ugumu kumuachia.

Vipers inashika nafasi ya pili kwenye ligi lakini msimu huu unaoendelea kinara wa mabao katika timu hiyo ni Okello mwenye mabao manane akizidiwa bao moja pekee na kinara wa ufungaji Ivan Ahimbisibwe wa URA SC.

Kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyewahi pia kuifundisha Vipers akizungumzia hatua hiyo ya Wekundu kumtaka Okello alisema, unaweza kuwa usajili mzuri kwani kiungo huyo ni mjuzi wa kutengeneza nafasi.

Robertinho, anayefundisha Rayon Sports ya Rwanda kwa sasa alisema, Simba inahitaji kukiboresha kikosi chake zaidi kwa kuleta wachezaji wenye uzoefu mkubwa na wabunifu.

“Namfahamu Okello sikumfundisha nikiwa Vipers, lakini namjua alikuwa timu nyingine, ni mchezaji mbunifu sana.”

Related Posts