Moshi. Unapoutaja Mkoa wa Kilimanjaro, wengi watauwaza Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu barani Afrika, uliobeba jina la Mkoa huo.
Hata hivyo, yapo mengi ya kujionea, mtu afikapo katika mkoa huo,ambao unatajwa kuwa na maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Mkoa huo wenye mandhari nzuri ya kuvutia, watu wenye ukarimu na utajiri wa utamaduni wa kipekee, licha ya kuishi makabila mbalimbali, ni chimbuko la kabila maarufu la Wachaga.
Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakiutofautisha mkoa huo na maeneo mengine na kuufanya kuonekana wa kipekee, ni utamaduni walioupa jina la kwenda kuhesabiwa, ambapo Wachaga hurudi nyumbani kujumuika kama familia, kusherekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Utamaduni huu umeufanya mkoa huo, kujipatia umaarufu mkubwa, katika kipindi cha Desemba, ambapo watu wa jamii ya wachaga walioko maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi, hurudi nyumbani ili kusherekea sikukuu na familia zao.
Wakati huo ni kipindi ambacho kumbi za starehe, baa na maeneo ya biashara, hushuhudiwa ongezeko kubwa la mauzo, watu wakifanya matumizi makubwa na ni kipindi cha kushuhudia magari ya kifahari yakipita katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Huko vijijini ni kipindi ambacho uchinjaji na kuchoma mbuzi (ndafu), unywaji wa pombe maarufu ya kienyeji ya mbege hushika kasi, lakini swali kubwa hapa nini kiini cha utamaduni huu na nini hufanyika vijijini watu wanapokutana?
Mwananchi imefunga safari hadi Kibosho katika kijiji cha Kindi na kuzungumza na mzee Tadeus Mushi (72) ambaye anasimulia uhalisia wa yale ambayo hufanyika wakati watoto wanapokuja nyumbani kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka
Mzee Mushi ambaye anaonekana kuwa mwenye hekima nyingi na ufahamu wa mambo ya kimila, anasimulia siri ya desturi hiyo adhimu na utamaduni huo wa familia na yale ambayo hufanya wakati wanapokutana.
Mushi anasema kipindi hicho ndicho ambacho hukutana ndugu jamaa na marafiki, baada ya kupotezana kwa mwaka mzima na kupanga mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka malengo ya mwaka mwingine.
“Ni wakati wa kula, kunywa, na kufurahi na familia, kufanya vikao vya familia kuweka mipango ya maendeleo,” anasimulia Mushi na kuongeza kuwa baada ya sikukuu, watu huanza kuondoka na kurejea kwenye shughuli zao.
Anasema mbali na kula na kunywa, wanaokuja kutoka safari hukaa na wazee na kuwaombea waliotangulia ili kupewa baraka kwa ajili ya mafanikio ya mwaka mwingine wanaokwenda kuuanza.
“Hapa nategemea pia watoto wangu wataanza kuja nyumbani kuanzia Desemba 20, tutajumuika pamoja kusherekea siku kuu na kuweka mipango mbalimbali ya maisha” anaeleza Mzee Mushi.
Anaongeza: “Lakini pia wanapokuja wanakaa na wazee wanakula kimbuzi halafu wanaomba kwa wazee na waliotangulia baba nikienda kule nifanikiwe zaidi na zaidi”
Anasimulia kuwa wakati wanawaomba, wazee husema “baba mbariki huyu atakapoondoka neema na baraka ziongezeke ili wakati mwingine akirudi huku, aje atupe tena chakula kingine kama hiki”.
Mzee Mushi anasema kipindi hiki mbuzi wengi huchinjwa na baadhi ya familia hutenga maeneo maalumu ya kuchinjia na kula.
“Kuna mahali maalumu pa kuchinjia mbuzi wakati huu, kuna wengine wanapenda wakae katikati ya boma, wengine wametenga eneo lenye majani ya Sale ambapo watu hukaa kula na kunywa na kupeana baraka ili kuuanza mwaka mwingine salama na baraka”
Anasema kutokana na utamaduni huo, wanaamini mtu asipokuja kukutana na wazee na kupewa Baraka, mambo yake hayatakwenda vizuri kama wenzake waliokutana na familia na kubarikiwa na wazee.
Mzee Mushi ambaye alikuwa shambani kwake akihudumia mbuzi, akidai wengine watatumika kama kitoweo wakati wa siku kuu, anasema hata hivyo, utamaduni wa familia kukutana umeanza kupotea katika baadhi ya maeneo kutokana na baadhi ya vijana kuupuuza na kukumbatia usasa, hali inayotishia kupotea kwa utamaduni huo wa asili.
“Mila hizi ni nguzo yetu. Vijana hawataki kusikiliza wazee, wanaenda na usasa, na huo ndiyo mwanzo wa matatizo ya kijamii,” anasema kwa msisitizo.
Sophia Makoi, mkazi wa Okaoni anasema katika kipindi hiki cha sikukuu, watu hukutana na watoto na wajukuu ambao hupata fursa ya kujifunza utamaduni wa kwao.
“Kipindi hiki ni muhimu sana kwani pamoja na kukutana na familia kupanga mipango ya mwakani, ni kipindi ambacho wajukuu wanakuja nyumbani kujifunza tamaduni za kwao na kuyafahamu mazingira ya asili walikotokea,’’ anaeleza.
Makoi ambaye alikuwa nyumbani kwake akiwafundisha wajukuu zake kazi za nyumbani, anasema utamaduni wa kukutana ni mzuri maana hutoa fursa ya wanafamilia kufahamiana na kubaini changamoto ambazo kila mmoja alipitia.
Anasema kwa sasa siyo wenyeji wa Kilimanjaro pekee wanaorudi nyumbani, na kwamba yapo baadhi ya makabila yameanza utamaduni huo ikiwa ni mpango wa kuimarisha umoja na mshikamano.
James Joseph, ambaye anaishi Dar es Salaam tayari amesafiri kwenda Kibosho kuungana na familia yake kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka, ambapo amesema kuna umuhimu wa kukutana kama familia kuweka mipango.
“Kipindi hiki cha mwisho wa mwaka tunafurahi kuja kuonana na wazazi na kujumuika kama familia. Tunakuwa hatujaonana mwaka mzima na sasa tunakutana kupanga maendeleo, “anasema
Mchungaji Glorious Shoo mwenyeji wa Machame, anapongeza utamaduni huo wa kukutana na kueleza kuwa, unapaswa kuigwa.
“Kwetu Wachaga kipindi hiki ni sikukuu kubwa, kwani wamekuwa na utamaduni wa kukutana kila mwaka, ni jambo la baraka. huu ni utamaduni mzuri na hili wanalolifanya ni zuri la kuigwa na ningetamani kila familia, kila koo kujenga utamaduni wa kukutana ili kufahamiana watoto wa mjomba shangazi na wengine”
Shoo anasema pamoja na mazuri ambayo hufanyika, zipo changamoto ambazo hukutana nazo, ikiwemo kupanda kwa gharama za usafiri, vyakula, nguo na bidhaa nyingine.