Dar es Salaam. Sasa ni rasmi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe atagombea tena nafasi hiyo akitarajiwa kukabiliana na Tundu Lissu kwenye uchaguzi wa mwenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika Januari 2025.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mbowe kutangaza msimamo huo, baada ya kutafakari kwa saa 48 alizojipa na kisha kusema kuwa atagombea tena nafasi hiyo na kwamba bado yupo Chadema na atagombea ili kutetea nafasi hiyo.
Mbowe ameeleza hayo leo Jumamosi Desemba 21, 2024 wakati akitoa mrejesho wa saa 48 alizokuwa akitafakari kuhusu ombi la wenyeviti wa Chadema wa mikoa 24 waliokwenda nyumbani kwake Desemba 18, 2024 kumuomba awanie nafasi hiyo kwa mara nyingine.
“Nimetafakari kwa kina sana, nimesema mara nyingi, nilitamani kuondoka, lakini siwezi kuondoka katikati ya minyukano iliyopo. Kwa hiyo, Chadema nipo, nitakuwepo, nitagombea. Mimi na viongozi wenzangu wote wanaoniunga mkono na wasioniunga mkono.Naamini tutakutana kwenye mazungumzo ya kukiweka chama chetu sawa.
“Kila mmoja apewe haki ya kugombea, anayetaka kugombea tukutane kwa box (sanduku la kura), tufanye kampeni za kistaarabu, nimewaambia viongozi wa mabaraza ya vijana, wanawake na wazee, kila mmoja afanye kampeni zake akijua ana wajibu wa kukilinda chama,” amesema Mbowe.
Katika maelezo yake, mwanasiasa huyo mkongwe, amesema kushambuliana kwenye uchaguzi kwa mambo yasiyokuwa na msingi, sio jambo linalojenga afya ya taasisi, amewaomba wanaomuunga na wasiomuunga mkono, kutambua anaheshimu haki yao.
“Haki yao hiyo haiwapi uhuru wa kunitukana, wala wasifikiri wana mamlaka ya kutukana mtu yeyote au kudhalilisha mtu yeyote kwa mambo ya uongo.Hatuwezi kujenga taasisi inayoheshimiana, inayojengwa kwa misingi ya kufitiana, kudhalilishana na kutimiza kazi inayofanywa na wengine,” amesema.
Mbowe ambaye ni mbunge wa zamani wa Hai mkoani Kilimanjaro, ametumia nafasi hiyo kuyaomba makundi yote ndani ya Chadema kufanya kampeni za kistaarabu za kujenga chama hicho kikuu cha upinzani.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alimuuliza swali Mbowe kama anamuogopa Lissu.
Amejibu kuwa: “Kuna mgombea anaitwa Tundu Lissu aliyekuwa makamu wangu simuogopi. Hivi nisimuogope Magufuli (John- Rais wa awamu ya tano) aliyekuwa na majeshi, nitamuogopa Lissu? Hivi ninamuogopea Lissu nini?
“Lissu ni kiongozi mwenzangu tunaheshimiana na tumekuwa wote kwenye chama, tumefanya mambo mengi mazuri hatuwezi kuogopana. Ila naamini mafahali wawili wanapokuwa zizi moja, basi hata Biblia Takatifu, maandiko yanasema kura huamua ubishi, ngoja tukamalize ubishi na wananchi waamue,” amesema Mbowe.
Kauli hiyo ya Mbowe haina tofauti na ile aliyoisema Lissu, Jumatano Desemba 17, 2024 wakati akitangaza nia ya kuwania uenyekiti wa Chadema, akisema hamhofii Mbowe endapo akitangaza kuwania uenyekiti.
“Sina wasiwasi wowote akigombea hata kidogo, sijawahi kuwa mwenyekiti. Nisipochaguliwa nitakuwa sijawahi kuwa mwenyekiti wa chama, nikichaguliwa nitakuwa mwenyekiti wa nne wa chama hiki,” amesema.