Yunus: Mambo Safi Msumbiji | Mwanaspoti

KIUNGO Mtanzania, Yunus Abdulkarim, anayecheza soka la kulipwa Msumbiji akiwa na timu ya Nacala, ameelezea uzoefu alioupata msimu uliopita, alipocheza kwa mara ya kwanza Ligi ya Mocambola.

Yunus, aliyeonyesha kiwango cha juu uwanjani akifunga mabao matatu msimu huo, akiungana na wachezaji wengine muhimu wa Nacala.

“Msimu uliopita ulikuwa na changamoto nyingi, lakini ulikuwa na mafanikio makubwa. Nilikuwa na furaha kuweza kucheza katika ligi hii ya Mocambola kwa mara ya kwanza, na kufunga mabao matatu ilikuwa ni hatua kubwa kwa maendeleo yangu binafsi na pia kwa timu,” alisema.

Yunus alijiunga na Nacala Julai mwaka huu akitokea JKU ya Zanzibar na aliweka alama kubwa kwa kutengeneza nafasi saba za mabao na kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho kilichomaliza msimu nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi na pointi 24.

Kiungo huyo amesema alijivunia kufanya kazi na wachezaji wazoefu wa Msumbiji na kujifunza mbinu mpya za uchezaji zitakazomsaidia katika safari yake ya soka.

“Nilikuwa na malengo makubwa na nilijua kupata nafasi ya kucheza Mocambola ni fursa kubwa. Ni ligi yenye ushindani mkubwa, pia imejaa vipaji, hivyo nilijua nitajitahidi kutoa kila kitu uwanjani,” aliongeza.

Hapa Tanzania Bara, Yunus alicheza kwa muda katika timu ya Polisi Tanzania, pia alitoa mchango mkubwa akiwa sehemu ya timu ya taifa la vijana la Tanzania chini ya umri wa miaka 20.

Related Posts