Serikali yapata hasara ya Sh79 bilioni bunifu za vijana

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha Serikali inainua vijana kupitia bunifu zenye tija, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amekiri Serikali kuingia hasara ya Sh79 bilioni zilizotolewa kusaidia bunifu za vijana nchini.

Amesema hasara hiyo imesababishwa na vijana kuchukua fedha ili kuwekeza kwenye bunifu zao na baadaye wakashindwa kuendeleza bunifu hizo, ili kupata faida na kurejeshea fedha walizokopeshwa na Serikali.

Hayo yamebainishwa Desemba 20, 2024 kwenye sherehe za kilele cha wiki ya bunifu mbalimbali nchini, zilizofanyika Maktaba Kuu ya Chuo Kikuu cha Dar es Saalam.

“Kama Serikali tumefanya uchunguzi wa kuingia hasara hii, tukagundua tatizo ni ufuatiliaji mbovu wa mapendekezo ya bunifu hizo za vijana,” ameeleza Ridhiwani.

Amesema kwa sasa Serikali itafuatilia kila mradi uliombewa fedha ili kuhakikisha unakwenda kama ulivyotakiwa.

Ridhiwani amebainisha kwamba kama Serikali wanaunga mkono juhudi za Tanzania Startup Association (TSA),  katika kuhakikisha inaongeza uelewa kwa vijana kuhusu namna bora ya kuendeleza bunifu zao.

“Tunatoa nafasi kwa wabunifu katika kuonyesha bunifu zao na kisha wakapata nafasi ya kujifunza zaidi na zaidi ili kuongeza ujuzi wa kuingia kwenye soko la ushindani,” ameeleza waziri huyo.

Pia, amesema elimu hiyo ni mafanikio makubwa ambapo moja ya msaada wa Serikali, ni kusaidia bunifu huku wakifanya marekebisho sehemu zenye upungufu.

“Tunafuatilia kujua maeneo yenye upungufu ili tutatue na tutengeneze mazingira mepesi ya vijana kufanikiwa katika eneo hilo,” amesema.

Kadhalika, Waziri huyo amesema ni jukumu la Serikali kuwatia moyo wabunifu wadogo bila kukataa tamaa ili waweze kukidhi maisha yao ya baadaye.

Ridhiwani amesema hajisikii vizuri kusikia vijana anakosa mtaji wa kuendeleza bunifu walizonazo.

“Serikali inaendeleza harakati za kuwekeza fedha nyingi ili kukuza bunifu, upungufu upo kwa watekelezaji wa majukumu haya, kwa kutowapa vijana taarifa muhimu kuhusu fursa zinazopatikana serikalini,” ameeleza.

Amesema kuna mfumo wa vijana ambao umelenga kusaidia bunifu change,  lakini vijana hawa hushindwa kukuza bunifu zao kwa madai ya kukosa mtaji.

“Kuna vijana wengi wanashindwa kufanikisha bunifu zao kwa kukosa fedha za kununulia vifaa, ni jukumu la Serikali kufungua milango na kutengeneza mazingira mazuri hata kwa watu binafsi kuwasaidia vijana hao,” amesema.

Ameeleza kuwa, ni ngumu mtu binafsi kutoa msaada ikiwa haoni mlango wa wao kuwasaidia vijana wenye bunifu hizo hapa nchini.

“Kama Serikali tunaendelea kuwapa watu binafsi moyo wa kuwasaidia vijana na Serikali inatengeneza mazingira mazuri ya wawekezaji na wawezeshaji kuungana na Watanzania ili kuhakikisha kuna mafanikio katika ubunifu,” ameeleza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TSA, Zahoro Muhaji amesema maonyesho hayo yalifanyika sambamba na majadiliano mbalimbali kuhusu namna ya kuinua bunifu changa.

“Tunahitimisha maonyesho haya kwa kuishukuru Serikali kwa kuunga mkono juhudi mbalimbali za vijana katika kukuza bunifu zao,” ameeleza.

Muhaji amesema kupitia taarifa za kimataifa kwa miaka minne sasa bunifu ndiyo sehemu pekee inayoongoza kwa kulipa kodi, kuzalisha ajira na kuvutia uwekezaji wa Dola za Marekani 300 milioni nchini Tanzana.

“Hizi ni fedha zilizoletwa Tanzania kama uwekezaji,” ameeleza Muhaji.

Mkurugenzi huyo amesema kwa tafiti zilizofanywa na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Costech), bunifu ndiyo sehemu pekee iliyozalisha ajira 100,000.

Related Posts