BAADA ya kuwa katika Tano Bora ya timu zilizoruhusu mabao machache duru la kwanza JKT Tanzania inaendelea kujiimarisha eneo la ulinzi imetuma ofa Coastal Union ikimhitaji Miraji Abdallah.
JKT ipo nafasi ya nane katika msimamo baada ya kucheza mechi 14, ikishinda nne, sare saba na kufungwa tatu imeruhusu nyavu zake kutikishwa mara nane nyuma ya kinara Simba ambaye amefungwa mabao matatu, Yanga sita, Azam FC saba na Singida Black Stars tisa.
Timu hiyo ya maafande imeiandikia barua Coastal ikiwajulisha inamhitaji Miraji ambaye ni nahodha wa timu hiyo akiwa amebakiza miezi sita kumaliza mkataba na timu hiyo.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya JKT Tanzania kimeliambia Mwanaspoti mazungumzo baina ya pande mbili yanaendelea kuangalia uwezekana wa kunasa saini ya beki huyo wa kushoto.
“Ni mchezaji ambaye anaruhusiwa kuzungumza na timu yoyote kutokana na mkataba wake kwa mujibu wa kanuni kumruhusu lakini tumeandika barua kwa viongozi wa Coastal Union,” alisema mtoa taarifa huyo.
Wakati huo huo kocha wa JKT Tanzania, Ahmed Ally baada ya kuambulia sare dhidi ya Namungo amesema suluhu tatu mfululizo zinampa pointi tatu lakini anakazi kubwa ya kufanya ili wachezaji wake waweze kutumia nafasi wanazotengeneza.
JKT Tanzania ilianza na suluhu dhidi ya Pamba Jiji, Mashujaa zote kwenye uwanja wao wa nyumbani ambao wana rekodi ya kuto kupoteza na juzi na Namungo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ahmed alisema ni nzuri kwasababu wanaambulia pointi moja tofauti na kupoteza kabisa lakini haina afya kwao kwani wanatengeneza nafasi wanashindwa kuzitumia.
“Mchezo ujao ni ugenini tena dhidi ya Simba nitafanyia kazi mapungufu niliyoyaona hasa safu ya ushambuliaji kabla ya mchezo wetu na Simba ambao sitarajii urahisi.”