Wasanii watakiwa kutumia sanaa kufikisha elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza

Wasanii wametakiwa kutumia sanaa kufikisha elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo katika jamii inayowazunguka.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayofanyika katika Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe jengo la Mkapa Health Plaza jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kisenge alisema kambi hiyo imefanyika kwa ushirikiano na Bodi ya Filamu Tanzania na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kuwafikishia huduma za kibingwa wasanii kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi kufikia mwisho wa mwezi Januari 2025.

“Wasanii wamekuwa kioo katika jamii yetu, tukaona ni wakati sasa kuwatumia ili waweze kutusaidia kuielimisha jamii namna ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo kwani magonjwa haya yamekuwa yakichangia vifo vingi duniani”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema wasanii wanapoyaelewa magonjwa hayo inasaidia kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia njia mbalimbali za sanaa ikiwemo maigizo, muziki na sanaa nyinginezo.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Gervas Kasiga alisema limekuwa jambo la kipekee mwaka huu wasanii kufunga mwaka wakiwa wamefanya uchunguzi wa afya zao na kupata elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Dkt. Gervas aliwataka wasanii kutumia fursa hiyo kwa umuhimu kwani nafasi kama hiyo huwa haijitokezi mara nyingi hivyo pale inapojitokeza inapaswa kutumiwa vizuri na kwa maslahi binafsi.

“Kupitia upimaji huu unaotolewa kwa wasanii itatusaidia katika tasnia kujua afya zetu ili tunavyoenda kufanya kazi zetu tuweze kuzifanya kwa ubora kufikia matarajio yetu na matarajio ya nchi yetu”, alisema Dkt. Gervas

Naye msanii wa bongo movie na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steven Mengele amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa hiyo kwa wasanii kupima afya zao.

“Taifa lenye watu dhaifu linaweza kukosa watu wenye fikra za kulijenga, lakini taifa lenye watu jarisi uongozwa na watu wenye afya imara hivyo kupitia fursa hii wasanii tusiipuuze tujitokeze”, alisema Steven

Steven alisema watu wengi wakiwemo wasanii wamekuwa wakitembea na maradhi bila ya wao kujijua kutokana na kutokuwa na mazoea ya kufanya uchunguzi wa afya hadi pale changamoto za kiafya zinapojitokeza.

“Tumepata fursa hii kama wasanii tukiwemo wasanii wa bongo flavor, bongo movie, washereheshaji (MC), wanamichezo mbalimbali kupima afya zetu, Tunamshukuru Rais Dkt. Samia ametusaidia tufunge mwaka 2024 tukiwa na afya bora bila ya kutumia fedha kupima afya zetu”, alisema Steven

Akitoa shukrani zake msanii wa bongo movie Devotha Mbaga amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwathamini wasanii na kuwapa fursa ya kupima afya ya moyo bila gharama.

“Moyo ndio injini ya mwili wa binadamu hivyo ukipata shida ya moyo lazima mwili wote utakuwa dhoofu ndio maana nilipoona nafasi hii nilifika mapema kufanya uchunguzi na kupata elimu ya namna nitaweza kujikinga na magonjwa ya moyo”, alisema Devotha

Devotha alisema huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo zinaweza kumfanya mgonjwa asijione kama yupo hospitali kwani wataalamu katika maeneo yote wamejipanga kutoa huduma na kumfanya mgonjwa ajisikie huru.

“Toka nifiki hapa nimepata huduma zote bure na baada ya vipimo kuonyesha kuwa na changamoto kidogo nimepewa dawa bila gharama, nawashukuru sana”, alisema Devotha

 

 

Related Posts