Tanesco lawamani katikakatika ya umeme  Toangoma

Dar es Salaam. Wakati wakazi wa Toangoma, Dar es Salaam wakilalamikia kukatika umeme mara kwa mara, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema uchakavu wa miundombinu ni sababu ya hali hiyo.

Kwa mujibu wa Tanesco, juhudi zinaendelea kufanyika kuhakikisha maboresho yanafanyika kutatua changamoto hiyo.

Maelezo ya Tanesco yanatokana na malalamiko ya wananchi wa eneo hilo, waliosema kukatika kwa umeme kunawaathiri.

Akizungumza mbele ya maofisa wa Tanesco waliotembelea eneo hilo kusikiliza na kutatua kero cha wananchi leo Desemba 21, 2024, Mkazi wa Toangoma, Sufa Badili amesema hali hiyo inasababisha vyakula kuharibika.

Amesema kwa sasa hawana uhakika wa kuhifadhi vyakula kwa mwezi, kwa hofu ya kuharibika kutokana na kukatikakatika kwa umeme.

Amesema umeme hukatika pasipo Tanesco kutoa taarifa za sababu ya hali hiyo.

“Toangoma wengi ni wajasiriamali wadogo, tumekuwa tukiishi kwa kujishughulisha, sasa mtu anaweza kununua bidhaa zake za Sh2 milioni umeme ukikatika zinaharibika ataishije na watu wanakuwa na mikopo,” amesema.

Mkazi wa Toangoma Malela, Yusuph Badi amesema kukatika kwa umeme imekuwa changamoto ya muda mrefu ambayo inahitaji kufanyiwa kazi.

“Tulipoambiwa mradi wa Mwalimu Nyerere wa umeme unajengwa utaondoa kero tulikuwa na matumaini lakini sasa bado, umeme unaweza kukata mara tano ndani ya saa tatu,” amesema Badi.

Abdallah Mahiga, ameeleza ukuaji wa makazi katika eneo hilo ndiyo umesababisha kuwapo kwa tatizo la umeme.

Hiyo ni kutokana na alichoeleza transfoma zilizokuwapo zililenga kukidhi nahitaji ya wakati huo, lakini sasa yameongezeka.

“Sasa ongezeko la watu limeongeza mzigo kwa transfoma zilizokuwapo, lakini baadhi zimeanza kubadilishwa na zimebaki chache ambazo zikibadilishwa zinaweza kuimarisha upatikanaji wa umeme, Tanesco wanajitahidi kukabiliana na hali hii ila sehenu nyingine bado,” amesema Maiga

Akijibu malalamiko hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco Kigamboni, Julius Maira amesema ukongwe wa eneo hilo umesababisha miundombinu yake kuwa chakavu.

Hata hivyo, amesema wapo katika hatua ya kuifanyia maboresho ili kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika.

“Eneo la Feri nao walikuwa na changamoto kama hizi lakini tulianzisha miradi iliyotatua changamoto hiyo na sasa tunahamia Toangoma.

“Kero hizi zitatusaidia tunapofanya matengenezo tuwe na uhakika wa tunachofanya. Jumatatu (Desemba 23) ndiyo timu zetu zitaingia Toangoma kufanya matengenezo makubwa ili kutatua changamoto kubwa zinazowakabiki wananchi,” amesema Maira.

Wakati hilo likifanyika amesema anaamini hali itatengamaa zaidi pindi transfoma ya Mbagala itakapowaka kwa sababu itasaidia kupunguza baadhi ya wateja wa Kigamboni kwenda Mbagala ili wapate uhakika wa umeme.

“Pia siku ya Jumatatu miongoni mwa yatakayofanyika ni kubadili nguzo za umeme chakavu, kukata miti ambayo imekuwa ikisonga miundombinu ya umeme ili kuwahakikishia wananchi huduma,” amesema.

Hali inayowakabili wakazi wa Toangoma, ndiyo inayowasumbua wakazi wa maeneo mengine ya nchi.

Kinacholalamikiwa zaidi ni kukatika kwa umeme bila taarifa kutoka Tanesco hali inayoweka hatarini vifaa vya umeme, huku wafanyabiashara wakipata hasara.

Related Posts