Wamalawi 48 waliokuja kutafuta maisha, wapigwa faini ya Sh500,000

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu raia 48 wa Malawi kulipa faini ya Sh 500,000 au kwenda jela miezi sita kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kuishi nchini Tanzania bila kuwa na kibali.

Pia, Mahakama hiyo imeelekeza washtakiwa hao, baada ya kumaliza kutumikia adhabu hiyo, warejeshwe nchini kwao.

Washtakiwa hao ambao walidai kuwa wamekuja Tanzania kutafuta maisha, wamehukumiwa adhabu hiyo baada ya kukiri shtaka lao.

Hata hivyo, washtakiwa hao wameshindwa kulipa faini na hivyo wataenda kutumikia kifungo cha miezi sita jela.

Uamuzi huo umetolewa leo Desemba 20, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga baada ya kukiri shtaka hilo na Mahakama kuwatia hatiani washtakiwa hao.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Ruboroga amesema kosa linalowakabili washtakiwa hao, lina adhabu ya kifungo au faini au Mahakama inaweza kutoa adhabu zote kwa pamoja.

Amesema washtakiwa wametiwa hatiani kwa mujibu wa sheria kama walivyoshtakiwa baada ya kukiri shtaka lao na hivyo mahakama hiyo inawahukumu kulipa faini ya Sh500,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita jela kwa kila mmoja.

“Mahakama imetoa adhabu hiyo kwa kuzingatia washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza, wamekiri shtaka lao bila kuisumbua Mahakama na wameomba msamaha wa dhati mahakamani hapa,” amesema Hakimu Ruboroga.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, washtakiwa waliomba mahakama iwape adhabu ndogo kwani walikuja Tanzania kutafuta maisha.

Hakimu Ruboroga, baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili, aliwahukumu washtakiwa hao kulipa faini ya Sh500,000 kwa kila mmoja na wakishindwa kulipa faini basi watatumikia kifungo cha miezi sita jela.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Raphael Mpuya aliiomba Mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria.

Awali, akiwasomea maelezo yao, Wakili Mpuya akisaidiana na Hadija Masoud , alidai kuwa washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa lao Desemba 17, 2024 eneo la Mwananyamala, Wilaya ya Kinondoni.

Mpuya alidai kuwa washtakiwa hao waliingia nchini kupitia njia ya panya katika mpaka wa Kasumulu uliopo Kyela mkoani Mbeya na Songwe.

Alidai Desemba 17, 2024 saa 12:30 asubuhi, maofisa Uhamaji waliokuwa doria katika eneo hilo, waliwakamata washtakiwa hao kwa tuhuma za kuishi nchini bila kuwa na kibali.

Baada ya kukamatwa walifikishwa Ofisi za Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam na kuhojiwa ambapo walikiri kuwepo nchini na kwamba walikuja kutafuta maisha.

Washtakiwa baada ya kuhojiwa walifikishwa Mahakama na kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo, Desemba 17, 2024, saa 12:30 asubuhi eneo la Mwananyamala.

Inadaiwa siku hiyo, washitakiwa hao wakiwa wakiwa raia wa Malawi, walikutwa wakiishi nchini bila kuwa na kibali au nyaraka yoyote inayoonyesha uhalali wa wao kuishi nchini.

Related Posts