Songea. Stendi ya mabasi inayojengwa katika Kijiji cha Lundusi kilichopo Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, inatarajiwa kumaliza adha ya usafiri kwa wananchi walishio vijijini wanaolazimika kutumia gharama kubwa kufuata huduma ya usafiri mjini Songea, zaidi ya kilomita 60.
Kutokana na umuhimu wake, wananchi wameitaka kamati ya ujenzi wa mradi wa stendi hiyo kukamilisha mradi huo kwa wakati kama walivyoagizwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).
Ujenzi huo unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), umefikia asilimia 78 huku wananchi wakieleza kuwa ujenzi huo utakapokamilika, utaondoa changamoto ya usafiri kwa wananchi pamoja na kuimarisha usafirishaji.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea mradi huo, mkazi wa kijiji hicho, Celina Kasembe ameeleza kuwa stendi hiyo ikikamilika itasaidia kuwapunguzia gharama za usafiri ambapo kwa sasa wanatumia zaidi ya Sh40,000 mpaka Sh80,000 kukodi usafiri wa teksi kupelekwa stendi kuu ya Songea kwa gharama kubwa.
Amesema wanaishukuru Tasaf kwa kuwaletea mradi huo kwani wanaamini uchumi wa wananchi utakua stendi hiyo ikikamilika na kuanza kufanya kazi ambapo amewataka vijana kuchangamkia fursa ya kufanya biashara.
Naye Henrick Haule, mkazi wa Kijiji cha Lundusi amesema mradi wa ujenzi wa stendi, utatoa fursa kwa wananchi hususani vijana na kina mama kufanya biashara na kujiongezea kipato na wengine kupata ajira za ufundi.
Fundi mkuu wa ujenzi huo, Peter Mashine amesema mpaka sasa ujenzi huo umefika asilimia 78 na unatarajiwa kukamilika Januari 15, 2025 na kazi inaendelea kwa kasi inayoridhisha.
Mashine amesema ujenzi huo ulianza Agosti 2023 na utakapokamilika utakuwa na eneo la kuegesha mabasi, vyumba 36 vya biashara, matundu nane ya vyoo, jengo la utawala pamoja na jengo la ulinzi na usalama.
Ofisa Ufatiliaji wa Tasaf, Mlowe amesema wanatarajia mradi huo utakamilika Januari 2025 ili wananchi waanze kuonja matunda yake. Amesema wanatarajia stendi hiyo itawaondolea wananchi adha waliyokuwa wakiipata.
Akizungumzia mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hassan Mtamba amesema ujenzi wa stendi hiyo umelenga kuondoa changamoto ya usafiri kwa wananchi waishio maeneo hayo.
“Kituo hiki cha mabasi kitakapokamilika na kuanza kutoa huduma kitawaondolea usumbufu na gharama wananchi wa maeneo hayo ambao kwa sasa inawalazimu kuja mpaka Songea kupata huduma ya usafiri wa mikoani na maeneo mengine, tunaishukuru Serikali kupitia Tasaf kwa kutupatia stendi hii,” Amesema.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Lundusi, Imelda Mbawa amesema wananchi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani wanapata shida wanapotaka kusafiri kwenda mikoani na maeneo mengine.
Amefafanua kuwa wanatumia gharama kubwa, kwa mfano mwananchi wa kijiji hicho anapotaka kwenda Dar es Salaam, Iringa au Mbeya, anatakiwa kuondoka kwenda kulala Songea ili kesho yake apande basi, hivyo stendi ikikamilika hatutakuwa na kero hiyo.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mratibu wa Tasaf katika Halmashauri ya Songea, Hosana Ngunge amesema utekelezaji wa mradi huo wa stendi, umeibuliwa na wananchi wenyewe ambao walituma maombi .