Ramovic amchomoa straika mpya Yanga

KABLA ya kuondoka Yanga, kocha Miguel Gamondi alileta straika mpya na kujifua na kikosi cha timu hiyo kambini, Avic Town, akisubiri kusaini mkataba wakati huu wa dirisha dogo, lakini alichokutana nacho kwa kocha wa sasa, Sead Ramovic, huenda hana hamu nacho.

Gamondi alimpokea straika huyo kutoka Uganda na kujifua na mastaa wa timu hiyo ili kusubiri dirisha dogo apewe mkataba asaini, lakini mambo yameenda sivyo baada ya kocha huyo kutimuliwa baada ya Yanga kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya Azam na Tabora na kuletwa Ramovic.

Straika huyo aliyepigwa chini ya Ramovic ni  Fahad Bayo, raia wa Uganda aliyekuwa akijifua na kikosi cha sasa wakati akiangaliwa na Gamondi aliyetimuliwa mwezi uliopita baada ya Yanga kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya Azam (1-0) na Tabora United (3-1).

Wakati Ramovic akitua Yanga alikutana na Bayo akiendelea na mazoezi, lakini kocha huyo amewaambia mabosi wa timu hiyo, anataka mtu wa maana katika eneo hilo zaidi ya Mganda huyo kwani kwa kiwango alichonacho ha na tofauti na kila Clement Mzize, Prince Dube, Jean Baleke na Kennedy Musonda wanaotumika eneo hilo.

Ramovic amewaambia mabosi wa Yanga kuwa hataki historia anataka mashine zenye uwezo wa kukifanya kikosi chake kuwa rahisi.

Inaelezwa Bayo aliyetokea klabu ya MFK Vyskov ya Jamhuri ya Czech akiifungia mabao nane katika mechi 42  uzito wa mwili wake ndio umemfanya kocha huyo kumkataa, kwani ameonekana kibonge.

Tayari mshambuliaji huyo ameshatimka nchini kimyakimya akirudi kwao Uganda huku maisha ya kuanza kutafuta mshambuliaji mpya yakianza haraka.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti; “Mbona ameshaondoka (Bayo) alirudi kwao Uganda naona kocha mpya (Ramovic) amemkataa anataka mtu Bora mara tatu yake.”

“Mchakato wa kutafuta mshambuliaji mpya tumeshaanza na huyo anausimamia yeye mwenyewe kocha, unajua huyu ni kocha ambaye hataki kuangalia historia ya mchezaji nyuma kwamba alikuwa mzuri anataka kuona ubora wake uonekane sasa,” kiliongeza chanzo hicho kutoka Yanga.

Inaelezwa, kocha Ramovic bado anaendelea kuwasoma wachezaji wa sasa hususani washambuliaji ambao anapiga hesabu za kupangua eneo hilo, ambalo hadi sasa ni Dube ndiye anaongoza baada ya kufunga mabao matatu mechi iliyopita, huku Musonda na Mzize kila mmoja akifunga mawili, wakati huku Baleke akiwa na moja tu.

Related Posts