Uishije na wageni msimu huu wa likizo na sikukuu

Kipindi cha likizo ya mwisho wa mwaka baadhi ya familia hupokea ndugu zao kutoka sehemu mbalimbali wanaofika kwa ajili ya kusalimia.

Bila kujali idadi, uwepo wa wageni hawa huweza kubadilisha mfumo wa maisha wa familia husika kutokana na kuongezeka kwa bajeti inayotumika, hususan katika kununua chakula cha siku husika kuanzia asubuhi hadi jioni.

Uwepo wa ugeni huu kwa baadhi ya watu imekuwa ni changamoto kwao kutokana na hali ya uchumi wanayokuwa nayo kwa wakati husika, huku ukweli ukibaki moyoni kwa wenye nyumba kutokana na kutafuta kila namna ya kupambana kutimiza mahitaji ya msingi ya kila siku bila kuonyesha pengo lolote.

Lakini wakati mwingine hali huwa mbaya zaidi pale wageni wanapofika na utaratibu wao, ikiwemo kuchagua vyakula na wengine wanakwenda mbele zaidi kupanga mfumo wa maisha.

Jambo hili huwaumiza vichwa hasa wanawake, ambao ndio huendesha shughuli za nyumbani, ikiwemo kutunza familia na wengi wakiumiza vichwa ni kwa namna gani wanaweza kupita katika kipindi hiki bila kuathiri uchumi wa familia.

Katika baadhi ya familia, ikiwemo ya Elibariki John tayari zimeshuhudia kupaa kwa gharama za maisha baada ya wanafamilia kuongezeka.

John, akiwa na familia ya watu watatu na mtoto mchanga amepoke ugeni wa wazazi wawili na watoto sita na hivyo kumfanya kuwa na familia ya watu 11 ndani ya nyumba ya vyumba vitatu vya kulala na sehemu ya kulia chakula.

Anasema jambo hilo limebadili desturi ya familia yake ya kununua chakula cha Sh200,000 kwa ajili ya matumizi ya mwezi mzima ambayo ilikuwa ikiambatana na Sh7,000 kwa ajili ya kununua vitu vidogo vidogo kila siku.

“Hii akiba ya chakula ya Sh200,000 niliyokuwa nikiweka inatumika mwezi mzima na hiyo Sh7,000 ya nyanya na mbogamboga ilitosha, lakini sasa hilo haliwezekani, nalazimika kuacha Sh15,000 kila siku na kile chakula cha mwezi kimeliwa ndani ya wiki,” anasema John.

Anasema tangu apokee ugeni huo Novemba mwaka huu, zaidi ya Sh800,000 imetumika kwa ajili ya kuhudumia familia yake na wageni hao.

Wakati John akiyasema hayo, kwa Flackian John, mkazi wa Arusha ni tofauti, anasema ndani ya nyumba yake kuna baadhi ya wageni wakifika hubadili mfumo mzima wa maisha yao, ikiwemo wao kuamua aina ya vyakula.

“Mara nyingi wageni wanaokuja ni ndugu upande wa mume wangu, kipindi kama hiki tunakula kwa kutegemea ratiba za hao ndugu, yaani mama mkwe na mawifi,” anaeleza.

Anasema ndugu hao wana tabia ya kumfuata kaka yao na kumweleza aina ya chakula wanachokitaka.

“Baada ya kumwambia ndugu yao ndipo nipewe ratiba ya wao kula, ilibidi nimwambie mume wangu awe anawaachia matumizi wapike wanachokitaka wao, mimi sina tatizo,” ameeleza

 Anasema aina hiyo ya maisha ni kero kwake. “Kipindi kama hiki sijawahi kukifurahia kabisa, ndugu wana kero na gubu na wakati mwingine ni wachonganishi, natamani wasije ila sina jinsi, najikaza,” anasema.

 Unaishije ndani ya bajeti

Wakati kuongezeka kwa matumizi ikiwa ni moja ya kilio cha watu wengi, manunuzi ya jumla na kuandaa vyakula nyumbani, hususan kitafunwa kwa ajili ya chai asubuhi yanashauriwa.

Hali hii inatajwa kama njia mojawapo inayoweza kusaidia kupunguza makali ya maisha kutokana na kushusha gharama ya baadhi ya vitu.

“Ukinunua kitu kidogokidogo lazima utaona maumivu yake, ukinunua kwa jumla bei inapungua na unakaa muda mrefu bila kurudi dukani, unasahau maumivu na hii inakupa pia uhakika wa kula hata ukiwa huna hela,” anasema Winfrida Makame na kuongeza:

“Kama una watu wazima sita ukisema ununue maandazi walau manne kila mmoja ni Sh2,400, lakini baadhi ya wageni wetu hawashibi, ukisema ununue chapati 2 kwa kila mtu kama inauzwa Sh300 ni Sh3,600, sasa siyo kila sehemu andazi linauzwa Sh100 na chapati Sh300,” anasema Winifrida.

Anasema hiyo ni tofauti na mtu akiwa mtundu na kubadili vitafunwa, ikiwemo kuwapikia watu maandazi, chapati, viazi, mihogo huku akisisitiza kuwa kinachotakiwa ni kutokuwa mvivu.

Maneno yake yanaungwa mkono na Lucy Samson, ambaye anasema kujifunza kupika vitu nyumbani ndiyo njia pekee ya kuepuka gharama kubwa.

Anasema sehemu hii pia ndiyo ubunifu unahitajika katika kupika vitu vilevile kwa namna tofauti, huweza kusaidia kuondoa malalamiko ya watu kuchoshwa na chakula au mboga fulani.

“Unatumiaje viungo ulivyonavyo, nazi, karanga, katika kufanya kitu kiwe na ladha tofauti, watu wanaweza kusema hawataki maharage, lakini umeyapikaje ndiyo itaamua wale au wakatae, weka nazi, karanga, viungo si mafuta tu. Mihogo hawataki kaanga, viazi pika kachori hakuna atakayekataa,” anasema Lucy.

Anasema utundu pekee ndio unaweza kufanya maisha kipindi hiki kuwa rahisi na kumfanya mtu kuondokana na msongo wa mawazo juu ya kitu gani atawapa wageni wale waridhike.

“Ukishindwa sana wape wageni hela ya kula kama ni wanawake na wenyewe waumize kichwa watapika nini kwa hela waliyopewa,” anasema Lucy huku akicheka.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya hakuna kipimo mahususi kinachoangazia namna gani wageni wengi kwenye familia kinavyoweza kuathiri uchumi wa nyumba husika.

Mtaalamu wa Uchumi, Colman Njau anasema katika mtazamo wa kawaida familia nyingi zinazopokea wageni ni zile ambazo zina hali fulani nzuri kidogo kiuchumi.

“Hivyo pamoja na kuwa kuna gharama za kuhudumia wageni, lakini kuna faida ya kujumuika kama familia ambayo wale wanaoshindwa kuwwahudumia huikosa ni kubwa sana. Kwa sababu binadamu ni kiumbe hai, hivyo anatamani kukaa na jamii anayoendana nayo,” anasema Njau na kuongeza:

“Ni bahati mbaya hatuna kipimo cha uchumi kuangalia gharama za ndugu, jamaa, marafiki au wageni wanotutembelea, lakini wengi hujisikia faraja kupata fursa hiyo na hii ni kuashiria kuwa ni jambo linalothaminiwa na wahusika.

 Mwanauchumi Timoth Lyanga anasema kama kaya ni vizuri kuishi kwenye ile bajeti uliyoipanga na kuizoea.

“Kwa kipindi cha mwaka mzima familia nyingi zinakuwa na akiba walizodunduliza, akiba hiyo mara nyingi hutumika kwa matumizi ya dharura kama vile mafuriko, magonjwa na dharura nyingine nyingi,” anaeleza.

Anasema kaya inapopokea ugeni asiotarajiwa ni wazi gharama huongezeka na kisha kutumia akiba uliyojiwekea.

“Uwepo wa wageni hao, huiathiri familia katika suala zima la maendeleo kutokana na matumizi yasiyotarajiwa kipindi hiki cha sikukuu,” anasema.

Anasema kupokea ugeni huo kutafanya familia, kaya isione ile faida ya mwaka wala akiba aliyojiwekea.

“Matumizi ya fedha za akiba kipindi cha ugeni, huathiri maisha ya wakati ujao na hasa unapokutana na majanga ya asili au yasiyotegemewa utashindwa kujiokoa,” anaeleza.

Related Posts