MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Al Talaba ya Iraq, Simon Msuva amesema bado hajaingiziwa pesa zozote kutoka Wydad AC anazowadai.
Msuva aliishtaki Wydad Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kutokana na kushindwa kumlipa pesa za usajili ikiwemo malimbikizo ya mshahara Dola 700,000 sawa na zaidi ya Sh1.6 bilioni.
Akizungumza na Mwanaspoti, Msuva alisema bado anaendelea kusubiri kwani hadi sasa bado hajaingiziwa fedha hizo.
“Sina mengi ya kukuelezea lakini tuendelee kusubiri hadi sasa sijalipwa pesa yangu, hivyo Wydad imefungiwa kusajili wachezaji wa ndani ya Morocco nje na nje ya kimataifa hadi watakaponilipa pesa zangu,” alisema Msuva.
Julai 2022, Mshambuliaji huyo aliishtaki Wydad kwa kosa la kuvunja mkataba kinyume na utaratibu baada ya kuwa katika mvutano wa kimasilahi na vigogo hao wa soka la Afrika ambao walimsajili Novemba 2020 akitokea Difaa El Jadida ya Morocco.