Kilimanjaro. Hatimaye mwili Gilbard Mosha (41), umezikwa katika kitongoji cha Koniko B, kijiji cha Rauya, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro
Gilbard aliyekuwa fundi wa kuchomelea vyuma Tunduma mkoani Songwe, alifariki Novemba 27, 2024, kutokana na ajali kazini, lakini mwili wake ulishindikana kuzikwa mapema kutokana na mgogoro wa kifamilia kuhusu eneo atakalozikwa.
Mgogoro huo uliibuka baada ya upande mmoja ulitaka azikwe eneo la makaburi ya familia Koniko B, huku upande mwingine ukitaka azikwe katika eneo alilopewa na baba yake jijini Arusha.
Kwa siku 28 mwili wa marehemu ulikuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha jambo lililosababisha gharama za mochwari kuongezeka na kuleta changamoto zaidi kwa familia.
Upande uliotaka azikwe Koniko B, ambao ni mashangazi na bibi wa marehemu walikuwa wakisimamia hoja kuwa wazazi wake na ndugu zake wamezikwa hapo hivyo yeye hawezi kuzikwa nje ya eneo hilo, huku baba mdogo na mwanafamilia mwingine aliyejitambulisha kama msimamizi wa mirathi wakipinga kwa madai kuwa eneo hilo liliachwa kwa mdogo wa marehemu ambaye ni wa kike, hivyo wakimzika hapo kunaweza kuja kuibua mgogoro baina ya watoto wa marehemu na shangazi yao (Joan).
Endelea kufuatilia Mwananchi.