LICHA ya kuanza kwa kusuasua katika First League, nyota wa zamani wa Simba na Mtibwa Sugar, Henry Joseph Shindika amesema hana hofu yoyote kwani anajua mwisho wa msimu ataifikisha Moro Kids katika nchi ya ahadi.
Henry anayeinoa Moro Kids ameanza bila ushindi katika mechi tatu za kundi A kwenye First League akiambulia sare dhidi ya Magnet FC (1-1), Hausang FC (1-1) na Tunduru Korosho (0-0) na kushinda nafasi ya tano katika kundi hilo.
Katika mechi hizo tatu, vijana wa kiungo huyo wa zamani, wamefunga mabao mawili pekee na kuruhusu mawili huku wakivuna alama tatu, huku Nyumbu ikiwa kileleni na alama sita. Moro Kids ilitupwa nje ya Kombe la Shirikisho kwa kufungwa bao 1-0 na Pamba Jiji katika raundi ya tatu.
Kocha huyo aliliambia Mwanaspoti, anaamini safari yao kwenye michuano hiyo bado iko salama na inakwenda vizuri kwani baada ya kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho sasa nguvu yao wanaiwekeza kwenye ligi.
“Kwenye ligi tunatarajia kupata matokeo mazuri yaani hilo nikuhakikishie kwa sababu najiamini nina timu nzuri na tuna maelewano na jambo zuri tumepata changamoto nzuri kwenye shirikisho,” alisema Joseph na kuongeza;
“Tukianza vizuri kama ilivyo malengo yetu bila shaka mwisho wa msimu tutapanda daraja kwenda Ligi ya Championship, hivyo tuachie dakika 90 za mpira zitaamua.”
Alisema kuwa kikosi chake kwa sasa kinakabiliwa na udhaifu katika umaliziaji, na kwamba vijana wake wanahitaji muda kurekebisha tatizo hilo huku akiahidi kulifanyia kazi na kuliweka sawa.
“Timu yangu inabebwa na nidhamu ya mchezo bila kujali mpinzani wetu ana uwezo gani, na pia wachezaji wangu wanafuata maelekezo tunayotoa kwenye benchi la ufundi kwahiyo wanatusikiliza na tunakwenda vizuri,” alisema Henry aliyewahi kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.