BAADA ya kuona mapungufu kwenye baadhi ya maeneo, Yanga Princess inadaiwa imekamilisha usajili wa wachezaji watatu kutoka Get Program.
Nyota hao ni beki wa kushoto, Diana Mnally, Kiungo Protasia Mbunda na kipa Zubeda Mgunda ambao kabla ya kucheza Get Program waliitumikia Simba Queens.
Kama usajili huo utakamilika Yanga itakuwa timu ya kwanza kusajili wachezaji watano dirisha hili dogo baada ya ule wa Mukandayisenga Jeannine kutoka Rayon Sports ya Rwanda na Juliet Nalukenge raia wa Uganda.
Inaelezwa nyota hao watatu wapo huru baada ya kuvunja mkataba na Get Program ambayo haikuwalipa mishahara kwa takribani miezi mitatu mfululizo.
Hadi sasa taratibu zote za usajili zimekamilishwa wakisubiriwa kutambulishwa tu na tayari wapo kambini wakianza mazoezi na timu hiyo.
“Kwenye michezo saba tuliyocheza tumeona kuna mapungufu hasa kwenye eneo la kiungo mzuiaji, beki wa pembeni hiyo ndiyo ripoti iliyoletwa na kocha hivyo walioletwa ni kwa mujibu wa kocha,” alisema mmoja wa viongozi wa Yanga.
Hata hivyo, usajili wa Juliet umeingia dosari Yanga na mshambuliaji huyo ambaye alikuwa tayari kambini, inaelezwa ameondoka nchini na kurudi kwao Uganda baada ya timu hiyo kushindwa kumwingizia fedha za usajili kwa muda waliokubaliana.