KUNA siri kubwa nyuma ya mabao anayofunga kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya ambayo itawafunza wachezaji wengine kuzingatia baadhi ya mambo wanayoambiwa na makocha.
Mwanaspoti limebaini kwamba asilimia kubwa ya mabao yake (tisa) amefunga kipindi cha pili, machache akifunga kile cha kwanza na Mudathri amefichua siri iliyopo.
Sababu aliyoitaja Mudathir wanaporudi vyumbani, kitu kikubwa ni kusikiliza kwa makini maelekezo ya kocha ili kuhakikisha wanaziba upungufu ambao waliufanya kipindi cha kwanza, jambo ambalo limekuwa likimpa mafanikio makubwa.
Ukiachana na jinsi anavyozingatia anachoambiwa, jambo lingine ni kupenda kurudia kuangalia mechi kuanzia kipindi cha kwanza hadi dakika 90 ili kujua alikuwa na mabadiliko gani kiuchezaji.
“Tunapokuwa tunarudi vyumbani kocha anakuwa anatuambia kila mtu kitu anachotakiwa kwenda kukifanya ili kuhakikisha tunashinda mechi. Baada ya mechi pia anasema wapi tulifanya vizuri na wapi tuongeze umakini,” amesema.
“Pia nina tabia ya kuangalia nilichokifanya kipindi cha kwanza na nilichoongeza kipindi cha pili, ndio maana unaona nimefunga mabao mengi kuanzia kipindi cha pili.”
Mudathir amesema pia amekuwa akipewa majukumu maalumu na kocha Miguel Gamondi kila anapopata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza na hata akianzia benchi.
Amesema anafurahi namna ambavyo anaaminiwa na namna wachezaji wenzake wanafurahia anachofanya huku akidai kuwa hakuna timu ya kuwazuia kutwaa taji msimu huu kwani wanacheza kwa umoja na ushirikiano mzuri.
Mwanaspoti linakuletea mechi alizofunga Mudathir na dakika zake. Bao lake la kwanza na muhimu kwa Yanga kutokana na kuipa pointi tatu muhimu lilikuwa ni katika mchezo wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Namungo alipofunga katika dakika ya 88.
Kwenye mchezo huo uliochezwa Septemba 20, mwaka jana katika Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, Mudathir alianzia benchi.
Lakini, bao la pili kati ya tisa aliyoifungia Yanga lililoipa pointi tatu lilikuwa ni kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa uliomalizika kwa ushindi mabao 2-1. Wafungaji walikuwa Maxi Nzengeli na Mudathir upande wa Yanga huku lile la Mashujaa likifungwa na Emmanuel Mtumbuka.
Bao la ushindi na la pointi tatu kwa Yanga lilifungwa na Mudathir katika dakika ya 85 baada ya dakika 65 mzani kubalansi kwa timu hizo kufungana 1-1 ndipo alipowanyanyua mashabiki wa timu yake dakika za jiooni.
baada ya hapo Mudathir alipeleka kilio kwa Dodoma Jiji timu yake ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, dakika ya 86 akiunganisha mpira nyavuni akichongewa pasi na Nickson Kibabage.
Dakika ya 82 Mudathir aliwanyanyua tena mashabiki wa Yanga kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar ambao chama lake liliibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye uwanja uleule akipokea pasi kutoka kwa Stephane Aziz Ki.
Pia alihusika kuipa Yanga pointi tatu kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa ugenini bao likifungwa dakika ya 40 na Joseph Guede akiungansha pasi safi iliyochongwa na Mudathir.
MABAO MENGINE YA MUDATHIR
Yanga vs KMC- 3-0 alifunga mawili
Yanga vs Ihefu FC- 5-0 alisunga moja
Yanga vs KMC- 5-0 alifunga moja
Namungo vs Yanga- 1-3 alifunga moja