Dar es Salaam. Mamia ya wanawake wanachama wa Chadema, wameandamana kwenda ofisi za makao makuu ya chama hicho, wakimsindikiza Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe kurudisha fomu ya kuwania kutetea nafasi yake.
Mbali na kuandamana hadi Mikocheni, Dar es Salaam ziliko ofisi hizo, wanawake hao pia wamechanga fedha Sh1.5 milioni na kulipia ada ya fomu hiyo, ikiwa ni ishara ya kuonyesha kumuunga mkono Mbowe.
Mbowe anakuwa mwanasiasa wa pili kulipiwa ada ya fomu ya uenyekiti, kama ilivyofanywa kwa mpinzani wake katika nafasi hiyo, Tundu Lissu aliyelipiwa na mmoja wa wafuasi wa Chadema, Edgar Mwakabela.
Mwanasiasa huyo alichukua fomu hiyo ya kuwania uenyekiti jana Desemba 21, 2024 baada ya kutangaza uamuzi wa kugombea nafasi hiyo na leo, Desemba 22 ameirudisha.
Kwa hatua hiyo, ni rasmi sasa Mbowe atakabiliana na Lissu katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa ndani ya chama hicho, unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Kundi la wanawake hao liliongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) mkoa wa kichama Ilala, Nice Gusunte walianza maandamano hayo kutoka nyumbani kwa Mbowe na kutembea kwa miguu hadi zilipo ofisi hizo.
Hadi sasa waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo ya uenyekiti ni watatu ambao ni Mbowe, Lissu na Romanus Mapunda wote wanasubiri kura kutoka kwa wajumbe ili kushika wadhifa huo.
Hata hivyo, huenda idadi ya watakaojitosa kuwania nafasi hiyo inaweza kuongezeka kwa kuwa dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu bado liko wazi na mwisho wake ni Januari 5, 2024.
Msafara wa maandamano ya miguu ulianzia nyumbani kwa Mbowe hadi Ofisi za Makao Makuu ya Chama Mikocheni, Dar es Salaam na kupokelewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila.