YANGA leo imeendelea wimbi la ushindi baada ya kuifumua Tanzania Prisons kwa mabao 4-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku Prince Dube akitupia bao moja na kumfanya afikishe matano kupitia mechi tatu mfululizo zikiwamo mbili za ligi na mojua ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Watetezi hao walipata ushindi kwenye Uwanja wa KMC Complex, ikiwa ni wa pili mfululizo tangu waanze kuutumia uwanja huo kutoka ule wa Azam Complex, na kuifanya Yanga irudi nafasi ya pili kutoka ya tatu ikiishusha Azam FC inayolingana nao pointi 33, lakini ikiizidi uwiano wa mabao.
Katika mchezo huo, kocha Sead Ramovic alikianzisha kikosi kilichokuwa na mabadiliko makubwa kulinganisha na kile kilichoifumua Mashujaa kwa mabao 3-2, akiwatumia nyota wa kigeni wa tatu, viungo Khalid Aucho na Stephane Aziz KI walioanza sambamba na Prince Dube, huku waliosaliwa wakiwa wazawa.
Ramovic alimpumzisha Abubakar Khomeiny aliyetunguliwa mabao mawili mechi iliyoopita na nafasi yake kuzibwa na Abutwalib Mshery, huku mabeki wote wakiwa wazawa akiwamo Kibwana Shomary na Nickson Kibabage sambamba na Ibrahim Bacca na Dickson Job, huku Clement Mzize, Mudathir Yahya na Farid Mussa wakitumika eneo la mbele.
Katika mchezo huo, beki Ibrahim Bacca ameendelea kuonyesha kazi ya kufunga anaijua baada ya kutupia mabao mawili, likiwemo moja la mkono kama alilowahi kufunga Diego Maradona katika mechi ya Kombe la Fainali za Kombe la Dunia 1986 dhidi ya England.
Bao la kwanza lililokuwa la tatu kwa beki huyo wa kati lilikuwa tamu baada ya kumalizia mpira uliogonga besela uliotokana na shuti la friikiki ya Aziz KI dakika ya 42, kabla ya kuongeza jingine dakika ya 84 akimalizika kona ya Pacome Zouzoua aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Farid Mussa. Hata hivyo marudio ya matangazo ya runinga ya Azam, yalionyesha beki huyo akiutumbukiza mpira huo kwa mkono akiwa hewani, ambapo hata hivyo sio kipa wala mabeki wa Prisons walioonekana kulilalamikia na mwamuzi Abdallah Mwinyimkuu kuita kati.
Kukubaliwa kwa bao hilo kumemfanya Baka, kufikisha idadi ya mabao manne akilingana na Dube ambaye leo pia alifunga bao moja na kuwa wachezaji wanaoongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Yanga imefunga mabao 23 na kufungwa sita, wakati Azam ina mabao 22 na kuruhusu saba, lakini ni ushindi wa 11 kwa Yanga katika mechi 13 ilizocheza hadi sasa ikilingana na Simba inayoongoza ikiwa na pointi 34 na mabao 29 ya kufunga na kufungwa matano ikiwa ndio timu yenye ukuta mgumu na safu kali ya ushambuliaji.
Washambuliaji walioanzishwa kwa pamoja, Clement Mzize na Dube kila mmoja alifunga bao na kuboresha vibubu vyao vya mabao kwa msimu huu.
Mzize alifunga bao la kwanza la Yanga kwa mchezo wa leo, dakika ya 13 akimalizia pasi ya Dube, likiwa la tatu kwake msimu huu, kabla ya Mzimbabwe huyo naye kufunga bao lake la nne kwa msimu huu, lililokuwa la tatu katika mchezo wa leo sekunde chache kabla ya mapumziko akimalizia pasi ya Aziz KI aliyeonekana kucheza kwa utulivu mkuu tofauti na mechi zilizopita, japo aliendelea kupoteza mipira mingi kabla ya kutolewa kumpisha Shekhan Ibrahim.
Mbali na Aziz Ki, wengine waliotolewa kipindi cha pili ni Khalid Aucho aliyempisha Duke Abuya, Dickson Job, Mzize na Farid nao walitolewa kuwapisha Pacome, Bakar Mwamnyeto na Chadrack Boka.