Ni Neema, kilio bei ya vyakula, nguo zikipaa

Dar/ Mikoani. “Kulia au kucheka ni kupokezana,” ndivyo wanavyosema wafanyabiashara wanaokitumia kipindi cha msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka kama fursa ya kupata fedha mara mbili ya awali, huku kwa wanunuzi wakilalamika kupaa kwa bei za bidhaa hasa za vyakula na mavazi.

Mfumuko huo wa bei unakolezwa na sikukuu ya Krismasi inayoadhimishwa

Jumatano Desemba 25, 2025 na Mwaka Mpya.

Wakati maandalizi ya sikukuu yakiendelea, gazeti hili limezunguka masoko mbalimbali ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Kilimanjaro na kubaini mfumuko wa bei za bidhaa.

Miongoni mwa bidhaa hizo ni vitunguu saumu ambavyo kilo moja inauzwa Sh17,000 kutoka Sh7,000 ya awali katika masoko ya jijini Dar es Salaam.

Viazi mbatata vinauzwa Sh6,000 kutoka Sh3,500 kwa sado ndogo huku bei ya mchele ikiwa ni rafiki, kwa kuwa kilogramu moja inauzwa kuanzia kati ya Sh1,600 na 2,500 kulingana na ubora.

Mmoja wa wafanyabiashara wa viazi mbatata, Soko la Mbezi, Michael Joseph amesema nyakati hizi ni za wao kutengeneza fedha.

“Hiki ni kipindi cha fursa na sisi tunakitumia vizuri kutengeneza pesa, ikifika Januari mambo huwa magumu, hivyo kipindi hiki ndicho tunafidia mwezi huu,” amesema.

Katika masoko ya Ilala, Buguruni na Kariakoo yote ya Dares Salaam, pia bei za bidhaa zimepanda.

Baadhi ya wafanyabiashara wamesema bidhaa nyingi zilianza kupanda jana, zikiwa zimesalia siku nne kuadhimishwa Sikukuu ya Krismasi Desemba 25.

Katika masoko  ya Ilala na Buguruni, Mwananchi imeshuhudia kilo moja ya vitunguu maji ikiuzwa kwa Sh1,500 badala ya Sh1,200 ya awali huku sado moja ya nyanya ikiuzwa Sh4,500 kutoka Sh2,500 na viungo vya pilau paketi moja ya gramu 500 iliuzwa kwa Sh3,000 kutoka Sh2,000 ya awali.

Akizungumza na Mwananchi, mfanyabiashara wa nyanya katika Soko la Buguruni, Mariam Salum amesema bei ya nyanya inaendelea kupanda kadri sikukuu zinavyokaribia.

“Kila mwaka bei hupanda wakati wa sikukuu. Jana tulinunua nyanya kwa Sh40,000 (tenga), leo bei imepanda zaidi, na unaweza kuja kesho ukakuta imebadilika tena. Wateja wanapaswa kuwa tayari kwa mabadiliko haya, kwani upatikanaji wa nyanya kutoka mashambani umekuwa wa shida,” amesema Mariam.

Mfanyabiashara wa Soko la Ilala, Ashraf Islam amesema sado moja ya nyanya iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh2,500 na tenga kwa Sh30,000 siku za nyuma, bei inabadilika kila siku.

“Biashara ya nyanya haitabiriki. Wapo wateja wanaojua kuhifadhi mapema, lakini wale wanaosubiri sikukuu huwa wanakumbana na bei kubwa,” amesema Islam.

Kwa upande wa viazi mbatata katika Soko la Buguruni, mchuuzi Mohamed Abdallah amesema bei ya viazi imepanda kutoka Sh70,000 na Sh80,000 kwa gunia na sasa vinauzwa kati ya Sh90,000 na Sh100,000 kwa gunia.

“Wateja wetu wakubwa ni wauza chipsi. Kwa sasa ndoo kubwa tunauza kwa Sh22,000, huku kisado kikiuzwa Sh 6,500,” amesema Abdallah.

Kwa bidhaa za nyama, kilo moja inauzwa kati ya Sh11,000 na Sh12,000, huku kuku wa mayai wakifikia Sh16,000 kwa mmoja kutoka Sh14,000 wiki iliyopita.

Bei ya kuku wa broila imeongezeka kutoka Sh6,500 hadi kufikia Sh7,000.

Ally Bwelo, muuza kuku wa Ilala, amesema kuna uwezekano wa bei kupanda zaidi sikukuu inavyokaribia.

Upande wa viungo, wauzaji wa rejareja wamepandisha bei ya pakti kutoka Sh3,000 hadi Sh5,000, ingawa kilo bado inauzwa Sh40,000.

“Pilau haliliwi kila siku, lakini msimu wa sikukuu unaleta mabadiliko makubwa,” amesema Nyakamba Sekiboni, mfanyabiashara wa Kariakoo.

Mfanyabiashara wa nguo Kariakoo, Aneth Filbert amesema hivi sasa nguo nzuri ya mtoto inauzwa hadi Sh65,000 haijalishi ni jinsi gani.

“Zipo hadi za laki au zaidi. Kipindi hiki mambo yanabadilika, nguo ambayo kipindi cha kawaida utaipata kwa Sh40,000 au 45,000 sasa inaenda hadi 60,000 na nguo ya kawaida ya Sh15,000 sasa ni 25,000 hadi 30,000,” amesema Aneth.

Baadhi ya wateja wameeleza namna ongezeko la bei linavyoharibu mipango yao, wakibainisha ni changamoto kipindi hiki cha sikukuu.

Julitha Steven, mkazi wa Kigamboni, amesema, “sikukuu ni wakati wa kusherehekea na familia, lakini bei za bidhaa zimetufanya kufikiria upya mipango yetu. Labda tutapunguza idadi ya vyakula tutakavyonunua.”

Kwa upande wake Anneth Komba amesema, “juzi nilikuja kuulizia gauni la mtoto nikatajiwa Sh25,000, leo nimeambiwa Sh30,000. Muuzaji kaniambia bei hiyo niliyotajiwa mzigo uliisha. Nafikiria kuwatafutia watoto nguo za mtumba tu.”

Hali  ilivyo Kilimanjaro

Mkoani Kilimanjaro, bidhaa za vyakula zimepanda bei huku nyanya, vitunguu na mchele bei zikipaa zaidi.

Katika masoko maarufu ya Mbuyuni na Soko la Kati, kilo moja ya mchele iliyokuwa ikiuzwa Sh3,000 imepanda na sasa inauzwa kati ya Sh3,500 na Sh3,800.

Nyanya ambazo sado moja ilikuwa ikiuzwa Sh3,000 sasa ni Sh5,000, huku vitunguu vikiongezeka kutoka Sh3,500 na sasa inauzwa kati ya Sh6,000 na Sh7,000 kwa kilo moja.

Mfanyabiashara Mwajuma Ally amesema msimu kama huu wa sikukuu bidhaa huwa zinapanda bei.

“Mfano tenga moja la nyanya tunanunua Sh70,000 na wakati mwingine ukiuza fedha yake inaweza isirudi,” amesema Mwajuma.

Mnunuzi Ester Shayo ameiambia Mwananchi kuwa bidhaa zinapanda bei hali inayowaumiza hasa watu wenye kipato cha chini.

 “Serikali ina wajibu wa kudhibiti mfumuko huu hata kama ni soko huria, wananchi tunaumia,” amesema Ester.

Hata hivyo, katika masoko na maduka makubwa, msongamano wa watu wanaofanya ununuzi umeongezeka.

Katika masoko ya Soweto, Sido na Mwanjelwa jijini Mbeya, bei za bidhaa zimeongezeka.

Mfanyabiashara wa ndizi, David Mambo amesema awali mkungu mmoja wa ndizi ulikuwa ukiuzwa kwa Sh5,000 lakini tangu juzi, unauzwa kati ya Sh6,000 na Sh7,000 kwa bei ya jumla.

Mambo  amesema kwa rejareja mkungu wa ndizi unauzwa kati ya Sh13,000 hadi Sh15,000 kulingana na ukubwa wa ndizi.

Mfanyabiashara wa duka la nguo, Aziza Nsomba amesema: “Nguo inayotoka China ni tofauti na ya Italy. Bei inategemea usafiri, mipaka na gharama za ofisi tunazolipia.”

Wakati Nsomba akisema hayo, mfanyabiashara mwenzake, Melisa Sanga ameiambia Mwananchi kuwa, “kila mmoja anatumia kipindi hiki kama fursa. Sikukuu ya Krismasi ni ya mwisho wa mwaka na wafanyabiashara wanajua watu huweka bajeti kwa ajili ya manunuzi kwa hiyo na sisi tunapandisha bei tunajua wanunuzi wapo.”

Licha ya bidhaa za nguo kupanda bei, baadhi ya wakazi wa Mwanza wamenunua nguo na viatu kutoka kwa wauzaji wanaofanya punguzo (safisha duka).

Miriam Joseph amesema amepita madukani na kukuta bei kubwa, akaamua kugeukia kwa wanaotembeza nguo kwenye mikokoteni.

“Huku nimenunua tisheti moja kwa Sh7,000 na suruali Sh10,000 na wengine wanauza Sh15,000 tofauti na madukani,” amesema Miriam.

Naye Ester Faustine amesema kiatu kilichokuwa kikiuzwa Sh25,000 dukani, kwenye mikokoteni hiyo amenunua kwa Sh10,000.

Kwa upande wa vyakula, kilo moja ya mchele inauzwa kati ya Sh1,600 hadi 2,300, nyama Sh10,000 na nyanya moja Sh 100.

Mfanyabiashara wa viungo, Hawa Mchalumbi, amesema nyanya zimepanda bei kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Imeandikwa na Saddam Sadick, Devotha Kihwelu, Janeth Joseph, Timothy Lugoye na Imani Makongoro

Related Posts