Wezi waiba kengele kanisani, Askofu Bagonza atoa neno

Mwanza. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amelihusisha tukio la wizi wa kengele ya Kanisa la Ihembe mkoani Kagera na kukithiri kwa momonyoko wa maadili katika jamii.

Amesema kwa tukio hilo na mengine, Taifa linahitaji toba na kumrejea Mwenyezi Mungu.

Taarifa ya tukio la wizi huo, ilisambaa kupitia kipande cha video kilichomwonyesha askofu huyo akitoa taarifa ya kuibiwa kwa kengele hiyo inayokadiriwa kuwa na uzito wa kilo 70.

“Nimepata taarifa mbaya jana asubuhi kwamba kengele yetu ya kanisa la Ihebe imeibiwa…yaani jimbo la Ihebe..jimbo la wasomi bado wanaiba (waumini wanaitikia..kengele) huko ni kwenda mbele au kurudi nyuma? Kengele iliyowekwa ili kuwaita wezi waje kutubu sasa wezi wameiiba.”

“Nawasihi sana tuwaombee wezi ili hiyo kengele hata wakiuza fedha zikiwekwa mifukoni zipige kengele mpaka wairudishe..unaiba kengele ya kanisa!,” amehoji na kushangaa.

Baada ya taarifa hiyo, Mwananchi Digital leo Jumapili Desemba 22, 2024, ilizungumza kwa simu na Askofu Bagonza aliyesema tukio hilo limeacha maswali mengi yasiyo na majibu.

Amesema usiku wa Desemba 13, 2024, watu wasiojulikana walitumia kamba kupanda juu ya mnara mrefu ulikofungwa kengele hiyo na kuondoka nayo.

“Inaonekana watu hao walichora vema tukio hilo kwa kujiandaa kikamilifu kwa sababu licha ya mnara ule kuwa mrefu, kengele iliyoibwa pia ilifungwa vema kwa nati na imedumu kanisani hapo tangu mwaka 1967,” amesema Askofu Bagonza.

Amesema kengele iliyoibwa inakadiriwa kuwa na uzito wa zaidi ya kilo 70 na iliingizwa nchini kutokea Ujerumani.

“Tukio la wizi wa kengele kanisani ni kielelezo cha mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu….yaani tunaiba kura, tunaiba mitihani, tunaiba mali na fedha za umma. Kama Taifa tunahitaji toba na kumrejea Mungu,” amedai Askofu Bagonza.

Amesema awali wizi huo ulihusishwa na biashara ya vyuma chakavu, lakini taarifa nyingine zaidi zinasema walioiba walidhani kengele hiyo iliyotengenezwa kwa vyuma vya zamani ina aina nyingine ya madini yenye thamani.

Hata hivyo, amesema tayari taarifa za tukio hilo zimesharipotiwa katika Kituo cha Polisi cha Nyaishozi, kwamba hakuna askari aliyefika eneo la tukio badala yake walichukua maelezo na hata RB hawakutoa.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Brasius Chatanda ameahidi kufuatilia tukio hilo kwa wasaidizi wake kisha kulitolea taarifa kamili.

“Iliibiwaje? Kengele ya aina gani? Mazingira ya kuibiwa? Na kwa sababu nilikuwa bado kwenye ile ajali sijapata kwa usahihi… wakinipa nitarudi kwenu,” amesema Chatanda.

Kwa mujibu wa Askofu Bagonza, kwa sasa juhudi binafsi za kupeleleza na kuitafuta kengele hiyo kwa wauza vyuma chakavu zinaendelea.

Related Posts