MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)umekamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Upenja katika Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kazkazini Unguja, Visiwani Zanzibar.
Kituo hicho kimezinduliwa rasmi leo jumapili Tarehe 22.12.2024 na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Rahma Kassim Ali katika shamrashamra za maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kukamilika kwa kituo hicho chenye thamani ya shilingi milioni 342, kutapekelea kuboreshwa kwa upatikanaji wa huduma za afya muda wote kwa wakazi wa Upenja na shehia za karibu.
Akizungumza mara baada ya kuzindua kituo hicho, Mhe. Rahma Kassim Ali, aliipongeza TASAF kwa juhudi kubwa inazofanya katika kuboresha maisha ya wanufaika wa mpango na jamii kwa ujumla kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Alisema, TASAF imekuwa na mchango mkubwa katika kuinua hali za maisha na kipato kwa jamii nzima kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, na kuwasihi wananchi wa Shehia ya Upenja kutunza miundombinu uliyojengwa ili idumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya wananchi wengi.
“Tunaishukuru na kuipongeza TASAF kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo huu wa kituo cha Afya Upenja, Kituo huki ni muhimu sana kwani kitasaidia upatikanaji wa huduma zote muhimu za afya kama vile upasuaji, huduma za kinywa na meno, Mama na Mtoto, huduma ya wagonjwa wa nje na huduma ya mionzi,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Shedrack Mziray, Mkurugenzi wa Mifumo, Tathmini na Mawasiliano wa TASAF Japeht Boaz alisema jumla ya shilingi bilioni 15.18 zimetumika katika utekelezaji wa miradi ya mbalimbali visiwani Zanzibar.
Kati ya hizo, zaidi ya shilingi bilioni 1.9 zilitumika katika kununua vifaa vya utekelezaji na shilingi bilioni 13 kilitumika kulipa ujira kwa kaya za walengwa zaidi ya 35,000.
“Miradi iliyotekelezwa ni katika sekta ya afya,vmaji elimu mazingira misitu, barabara, uvuvi, kilimo umwagilaiji na muindombinu,” alisema.
Aliongeza kuwa, katika kipindi cha Pili, TASAF imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi 15 ya kuendeleza miundombinu katika sekta ya elimu, afya na maji, ambayo imegharimu zaidi ya Shlingi bilioni 3.1.
“Kwa mwaka huu 2024, miradi mitatu yenye thamani ya shilingi milioni 750 imetekelezwa na kukamilika kwa upande wa Unguja katika shehia za Bambi, Kizimkazi dimbani na Upenja, Miradi mingine inaendelea kutekelezwa katika shehia za Donge, Uzi na Kizimkazi dimbani kwa jumla ya shilingi milioni 306.6.” aliongeza.