Ujumbe mzito wa maaskofu salamu za Sikukuu ya Krismasi

Moshi. Maaskofu wa madhehebu matatu tofauti, wameibuka na mambo 10 katika salamu zao za Krismasi 2024 huku suala la utekaji, kupotea kwa watu na mauaji likitawala salamu hizo.

Mbali na hilo viongozi hao wa dini wameonya  juu ya damu inayomwagika pasipo na hatia.

Katika salamu zao hizo walizotuma kwa waumini na Mwananchi kupata nakala, maaskofu hao ambao ni pamoja na Dk Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wametaka hatua zichukuliwe haraka.

Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa hilo, Dk Msafiri Mbilu amewataka Watanzania kusherehekea sikukuu hiyo huku wakiiombea nchi na kipekee kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa 2025.

Suala la watu kutekwa na kupotea, limegusiwa pia na Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki, Emmaus Mwamakula, ambaye ameapa kukemea maovu hata kama kwa kufanya hivyo atahatarisha maisha yake.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Askofu Oscar John Olotu ameenda mbali na kuitaka jamii kufahamu kuwa siku zote katika maisha, damu inayomwagika pasipo hatia huwa inadai kila mara.

Krismasi ambayo pia hujulikana kwa jina la Noeli, ni sikukuu ambayo Wakristo wengi husherehekea kuzaliwa kwake Yesu Kristo zaidi ya miaka 2,000 iliyopita na kwa kawaida husherehekewa duniani kote Desemba 25 ya kila mwaka.

Katika kipindi hicho, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo duniani, huitumia siku hiyo kutoa matamko mbalimbali kuelimisha au kukemea mambo ambayo hayampendezi Mungu katika nyanya za kidini, kijamii na kisiasa.

Walichokisema Askofu Mbilu, Bagonza

Askofu Mbilu, aliwataka waumini wa kanisa hilo na Watanzania kusherehekea sikukuu ya Krisimazi mwaka huu kwa kutubu dhambi na kuacha yale yote ambayo hayampendezi Mungu.

“Tusherehekee Krismasi kwa kufanya matendo ya huruma tukiwasaidia wasiojiweza katika maeneo yetu mfano watoto yatima, wajane, wagonjwa na wafungwa,”amesema Askofu Mbilu katika salamu hizo na kuongeza kuwa:

“Tusherehekee Krismasi kwa kupinga na kukemea maovu ya kila aina katika jamii kama vile ukatili wa kijinsia, mauaji, watu kutekwa, wizi na ujambazi.”

Askofu Mbilu amewataka waendeshaji wa vyombo vya moto kama pikipiki na magari, watii sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazopoteza maisha ya watu wengi, hivyo kupunguza nguvu kazi ya Taifa na Jamii.

Katika salamu zake Krismasi itakayoadhimishwa Jumatano Desemba 25, 2024 alizowatumia waumini wote wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, Askofu Bagonza amezungumzia masuala matano ya kijamii likiwamo la utekaji na watu kupotea.

“Habari za masikini kutajirisha matajiri si ngeni kwetu. Tumewaona wakulima masikini wakitajirisha matajiri, waumini masikini wakitajirisha wahubiri, Bodaboda masikini wakiwatajirisha wauza pikipiki na maaskari barabarani,” amesema askofu huyo.

Bagonza ameenda mbali na kueleza kuwa habari za wapiga kura masikini kutengeneza viongozi matajiri si ngeni pia miongoni mwa jamii ya Watanzania.

“Wakati huohuo hatuwaoni matajiri wanaowatajirisha masikini. Tunachokiona ni matajiri wanaodhani wana bidii na akili, masikini wanaoambiwa ni wavivu na hawana akili. Kwao hawa matajiri, kutajirika ni akili na ujanja.”

“Hawa matajiri huwaona masikini kuwa ni wavivu na wasio na akili lakini ukweli ni kwamba utajiri na umasikini vina uhusiano wa karibu sana na mara nyingi uhusiano huu umejengwa katika unyonyaji.

“Kuzaliwa kwa Yesu kulileta picha tofauti. Yeye alikuwa tajiri ili masikini wawe matajiri na alizaliwa katika hali ya masikini ili sisi tuwe matajiri. Masikini na matajiri wote wana nafasi katika kuzaliwa kwa Yesu Kristo,”amesema Askofu Bagonza.

Mbali na hayo, Askofu Bagonza amewataka waumini wamtazame Yesu kama mtu asiye mwanachama wa chama chochote cha siasa anayepoteza haki ya kuchaguliwa kuwa kiongozi na kuishia kuwachagua wengine wamwongoze.

Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Askofu Olotu katika salamu zake za Krismasi na mwaka mpya 2025, ameitaka jamii itambue kuwa Mungu anawawazia yaliyo mema kila wakati hivyo nao wawazie mema watu wote.

“Tuache vitendo vya unyanyasaji, dhuluma, chuki na uadui maana sisi sote tu waja wake Mungu na kwake tutarejea na kila mtu atakwenda kusimama mbele ya kiti cha hukumu kutoa hesabu ya kazi zake alizofanya wakati akiwa hapa duniani,” amesema.

Akizungumzia mambo ya mauaji, watu kupotea na kuuawa, Askofu Olotu amesema yanaumiza mioyo ya Watanzania wengi.

“Hebu tufikiri kwa makini, kama ni ndugu yako ametoweka au ameuawa utajisikiaje mpendwa je, kama ni baba ametoweka watoto wake au mke wake anasikia uchungu wa namna gani, jaribu kuvaa viatu vyao ujisikie itakuwaje,” amesema.

“Lakini tujue kuwa damu inayomwagika pasipo hatia inadai kila mara, tujifunze kwa Kaini ambapo Bwana alimwambia Kaini damu ya ndugu yako inanililia kutoka ardhini,” amesema huku akinukuu Biblia Mwanzo 4:10.

Hata hivyo, amewaomba viongozi wote wa dini wasiache kumwomba Mungu ili ainusuru nchi na majanga hayo na waombe pia kwa ajili ya viongozi wa nchi hususan Rais Samia Suluhu Hassan na safu yake yote. “Mungu awajalie Hekima na uadilifu.

Ujumbe wa Askofu Mwamakula

Ujumbe wa Askofu Mwamakula ulilenga katika mambo makuu sita ambayo ni pamoja na utekaji, kupotea na mauaji ya raia wasio na hatia, tatizo la ukosefu wa ajira, kupanda kwa gharama za maisha na gharama kubwa za matibabu.

“Tunaingia katika kusherehekea Krismasi wakati watu wetu wengi wapo katika hali ya mashaka, hofu hata kukata tamaa kwa mambo mengi sana,” amedai askofu huyo.

Amedai hali ya usalama kwa maisha ya watu na mali zao umezorota kwa kiasi kikubwa, vitendo vya utekaji na mauaji vimeiweka jamii ya Watanzania katika taharuki ambapo kadhaa wameuawa na watu wasiojulikana.

“Vijana wetu kadhaa waliotekwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita hawajulikani waliko. Pia, hali ya usalama wa majengo nchini inaogopesha, moto unaunguza majengo huku mengine yakiporomoka na uwezo wa uokozi ni mdogo sana.”

“Bidhaa bandia zinatishia hali ya afya huku kukiwa na hofu ya uwepo wa bidhaa zilizoisha muda wake madukani,”amedai Askofu Mwamakula.

Amesema ukosefu wa ajira nchini limekuwa janga linalotishia ustawi wa vijana. “Vijana wetu wengi waliohitimu katika shule, vyuo na vyuo vikuu wamejiingiza katika uhalifu wa aina mbalimbali kwa kukosa ajira ikiwemo wa mtandao.”

Mwamakula amesema uhalifu wa kisiasa unaonekana kuhalalishwa na watu wenye mamlaka kiasi cha kusababisha hata kufanyika kwa mauaji katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu, yamewakatisha tamaa vijana wengi,” amesema askofu huyo.

Amesema hata gharama za maisha nazo zimepanda juu kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa huku kipato kikiwa hakijaongezeka na  gharama za matibabu katika baadhi ya hospitali nazo ziko juu na wananchi wengi hawawezi kuzimudu.

Askofu Mwamamkula katika ujumbe wake, amezungumzia pia hali ya ubora wa elimu kwa Shule za Serikali akisema hauridhishi na kutaka juhudi zaidi ziongezwe ili kuzifanya ziwe bora zaidi.

Related Posts